Polisi yaonya kugusa waliouawa, waliojiua

JESHI la Polisi limeonya wenye tabia ya kuingia katika maeneo ya matukio, kushika au kugusa vitu vilivyotumika katika uhalifu.

Pia limeonya kushika watu waliouawa au kujiua kabla ya uchunguzi na kuitaka jamii kuacha haraka tabia hiyo kwani kasumba hiyo, huharibu uchunguzi na kuwaingiza katika kesi za jinai na mauaji.

Kamishina wa Polisi (Operesheni na Mafunzo), Awadhi Juma alisema hayo Dar es Salaam alipozungumza na HabariLEO kuhusu kasumba ya baadhi ya watu kuingia maeneo ulipotendeka uhalifu na kushika vielelezo kabla ya uchunguzi wa polisi.

“Watu waepuke tabia hiyo kabisa maana inaharibu uchunguzi hasa katika kuchukua alama za vidole na pia.

“Inawafanya wawe hatarini kushitakiwa wakihusishwa na uhalifu au mauaji hayo kwa kuwa alama za vidole vyao zitaonekana badala ya alama za wahalifu pekee,” alisema Awadhi.

Akaongeza: “Yanapotokea matukio ya kihalifu, watu wasiingilie eneo husika hadi polisi watakapofika na kumaliza uchunguzi wao; ukifanya hivyo, utaharibu uchunguzi na unaweza kuharibu ushahidi na hata kuhusishwa katika uhalifu huo”.

Awali katika banda la Polisi lililopo katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam katika Viwanja vya Julius Nyerere vilivyopo Temeke Dar es Salaam, Sajenti Samson Kasongi wa Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi wa Polisi makao makuu alisema katika maeneo mbalimbali polisi wanashindwa kupata taarifa sahihi.

Alisema pia wanakosa taarifa za kutosha kutokana na watu kuingia na kushika vielelezo zikiwamo silaha zilizotumika na kubaki au vitu vilivyoathirika au kudondoshwa katika tukio hilo la uhalifu.

“Kwenye tukio la mauaji, wananchi msishike wala kukanyaga vitu ili msiingizwe katika uhalifu huo badala yake, toa taarifa ili polisi waje na kukusanya taarifa muhimu za uchunguzi,” alisema Sajenti Kasongi.

Akaongeza: “Ukikuta mtu kauawa, usianze kumgusa au kushika vitu vilivyopo hapo kuonesha watu, subiri polisi waje ili usijiingize kwenye matatizo yasiyokuhusu”.

Msaki Theobald wa Kitengo cha Uchunguzi wa Matukio ya Kihalifu katika Jeshi la Polisi alisema katika maonesho hayo kuwa, polisi wanatoa hadhari hiyo kwa kuwa wahalifu wanaweza kuua mtu, kisha wakamning’iniza kama mtu aliyejinyonga na kuacha ujumbe ili kupotosha uchunguzi.

“Sisi hatuishii kuona amening’inia kuwa amejinyonga na eti tukaona karatasi ameacha ujumbe tukaamini hapana, tutafanya uchunguzi wa kina kwa vitu vyote vilivyohusika na kutumika mfano, kwenye kamba tutaangalia kama kuna vidole vya mtu mwingine au ni yule aliyekufa na hata hiyo karatasi, tutaichunguza,” alisema.

Akaongeza: “Tunaweza kuona kama kweli ndiye aliandika kabla hajafa, au imeandikwa na waliomuua hivyo, ukishika vitu hivyo, vidole vyako vitaonekana na wewe utahusishwa na mauaji hayo”.

Kumekuwa na matukio ya watu kukutwa wamekufa kwa kinachodaiwa kuwa ni kujinyonga huku wengine wakiacha ujumbe wa maandishi unaohusu sababu zake kujitoa uhai.

Habari Zifananazo

4 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button