WADAU wa masuala ya kisheria wameshauri Jeshi la Polisi nchini lisiache kutoa taarifa za matukio ya mauaji kwa sababu wananchi wana haki kupata taarifa kwa mujibu wa katiba ya nchi.
Hivi karibuni Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliagiza Jeshi la Polisi litumie busara katika kutangaza taarifa za matukio ya mauaji na ikiwezekana iache kutoa taarifa hizo kwa kuwa zinaongeza kasi ya vitendo hivyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, alisema ni muhimu wananchi wapate taarifa hizo kwa kuwa kutozitoa si suluhu ya tatizo.
Henga alilieleza HabariLEO kuwa taarifa za takwimu za matukio ya mauaji zinapotolewa zinasaidia kuelewa ukubwa wa tatizo na kutafuta njia mwafaka kulitatua.
“Naomba nitofautiane kidogo na spika ambaye pia ni mwalimu wangu na namheshimu sana. Lakini kwa kweli hapo ameteleza kidogo kwa sababu tatizo usipolisema haliondoki.
“Fikiria mauaji ya wenza yamefikia mpaka tunafanya tafiti sasa hivi, tukifunga mdomo tu tatizo litaendelea, watu wataendelea kuuana na tutajifanya hakuna tatizo kumbe tatizo lipo,” alisema.
Aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dk Rugemeleza Nshalla alisema Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kuwa mficha maradhi kifo humuumbua, hivyo njia ya kupambana na matatizo hayo siyo kuyaficha bali kuyasema ili jamii ijue hatua gani za kuchukua.
Dk Nshalla alisema Ibara ya 18 ya Katiba ya Tanzania inaeleza haki ya wananchi kupata taarifa, hivyo kuficha taarifa za matukio ya mauaji ni sawa mbuni anayeficha kichwa kwenye mchanga.
“Kwa hiyo dawa ya tatizo si kulikimbia bali ni kukabiliana nalo, kuficha ni kutaka watu wasijue kama wanauawa au ni kutaka kufanya watu wasijue nini kinaendelea. Kama kuna tatizo limetokea kwenye jamii tujue chanzo cha mauaji hayo ni kitu gani na tuchukue hatua za haraka za kukabiliana na vitendo kama hivyo,” alisema Dk Nshalla.
Alisema miongoni mwa hatua za kuchukuliwa kukabiliana na matukio hayo ya mauaji ni pamoja na serikali, wananchi, taasisi za dini na makundi mengine kushirikiana katika kutoa elimu kwa jamii, kuangalia makuzi yakoje badala ya kuficha taarifa.
Wakili wa kujitegemea, Reuben Simwanza, alisema japo inawezekana spika alilenga kuwalinda wananchi, kuwaepusha na taharuki au alitaka kuona namna taarifa zinavyotolewa zisiwafanye watu kuona kutoa uhai wa mtu ni kitu cha kawaida, lakini kwa dunia ya sasa si jambo zuri mtu kutaka watu wanyimwe taarifa.
Simwanza alisema katika dunia ya sasa, watu wanapenda kuona suala la upatikanaji wa taarifa linapigiwa chapuo au kuungwa mkono na watu kuhimizwa kupata taarifa kutoka katika vyanzo sahihi lakini pia watu wahimizwe kutoa taarifa sahihi.
“Haki ya kupata taarifa ni haki ya kikatiba, hivyo kumzuia mtu asipate taarifa si sahihi,” alisema Simwanza.