JESHI la Polisi leo linazindua kampeni ya mwezi ya kusalimisha silaha haramu hususani bunduki, bastola au bomu.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni anatarajiwa kuzindua kampeni hiyo katika Viwanja vya Mashujaa jijini Dodoma.
Mwawakili wa kujitegemea, Reuben Simwanza na Daniel Kalasha, walisema kuwa uamuzi huo wa Jeshi la Polisi ni jambo jema na uungwwe mkono.
Mawakili hao walisema miongoni mwa makundi yanayolengwa na kampeni hiyo ni watu wanaomiliki silaha za kurithi bila kuzingatia utaratibu wa kuzimiliki kihalali.
Kalasha alisema kisheria mmiliki wa silaha anapokufa, mrithi au familia ya marehemu inatakiwa kuisalimisha silaha hiyo polisi na kupewa nyaraka maalumu.
“Mmiliki wa silaha anapofariki, familia au msimamizi wa mirathi akiendelea kuishikilia, inahesabika kama silaha haramu hata kama katika wosia ametajwa kuwa mmiliki. Anatakiwa aisilimishe polisi na kuanza maombi upya ya umiliki wa silaha hiyo,” alisema Kalasha
Simwanza aliyataja makundi mengine yanayolengwa na kampeni hiyo kuwa ni wamiliki wa silaha ambao vibali vyao vya kumiliki vimeisha muda wake na hawajavihuisha.
Alisema kushindwa kuhuisha kibali cha kumiliki silaha kunawafanya watu hao kuwa siyo wamiliki halali, hivyo silaha hizo zinahesabika kama silaha haramu na zinapaswa kusalimishwa polisi.
“Kuna watu wengine wanaingia na silaha hapa nchini isivyo halali, inawezekana walikotoka wanamiliki kihalali, lakini wanapoingia nazo hapa nchini bila kufuata utaratibu zinakuwa silaha haramu, pia kuna watu wasio wema wakiwemo majambazi, nao wanamiliki silaha isivyo halali,” alisema Simwanza.
Kwa mujibu wa Simwanza, makundi hayo ni walengwa wa kampeni hiyo ya Jeshi la Polisi ya kusalimisha silaha kwa hiari.
Kwa kuwa kampeni hiyo itakuwa ya mwezi mmoja, Kalasha alisema baada ya hapo Jeshi la Polisi linaweza kuanza operesheni ya kuzisaka na kuzikusanya silaha haramu kwa kuwa wana taarifa za kutosha, hivyo hakutakuwa tena na fursa ya watu kujitetea.
Jana Jeshi la Polisi kupitia Msemaji wa Jeshi hilo, David Misime, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, alisema uzinduzi wa kampeni hiyo maalumu inayojulikana kama msamaha wa Afrika itahusu usalimishaji wa silaha haramu kwa hiari zinazomilikiwa na watu kinyume cha sheria.
Misime alisema baadhi ya watu hao wanamiliki silaha hizo ama kwa kutokujua taratibu za umiliki wa silaha au vinginevyo, hivyo wanawapa wito wa kuzisalimisha kwa kuwa kukaa na silaha hizo ni kosa kisheria.
“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kutambua kuwa suala la ulinzi na usalama ni la kila mmoja wetu na kila mtanzania mpenda amani anao wajibu wa kuhakikisha analinda amani ya nchi yetu kwani pasipo amani hata maendeleo hayawezi kupatikana,” alisisitiza Misime.
Misime alisema yeyote atakayesalimisha silaha anayomiliki kinyume cha sheria katika muda utakaotolewa na Waziri mwenye dhamana hatakamatwa, kubugudhiwa au kuulizwa jambo lolote.