Polisi yashikilia sita kwa mauaji ya mlinzi wa duka

WATU sita wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Pwani kwa tuhuma za mauaji ya mlinzi wa duka.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi,  Pius Lutumo alisema kuwa watu hao walimuua  mlinzi huyo kisha kuiba baadhi ya vitu kwenye duka hilo.

Lutumo alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 28, mwaka huu eneo la Lulanzi, Kata ya Picha ya Ndege, wilayani Kibaha.

Advertisement

“Watu hao walimvamia mlinzi huyo aliyetambulika kwa jina la Alex Patakiri (25) ambaye alikuwa akilinda duka la Paulo Mlay na kumuua na  kisha kuiba vitu mbalimbali,”alisema Lutumo.

Alisema kuwa  polisi kwa kushirikiana na raia wema kupitia taarifa za kiintelijensia waliweza kuwakamata watuhumiwa hao pamoja na vitu vilivyoibwa.

“Watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani ili kujibu tuhuma zinazowakabili mara baada ya upelelezi kukamilika,”alisema Kamanda Lutumo.

Aidha alisema kuwa walifanikiwa kuokoa mali za wananchi zilizoibwa maeneo mbalimbali ya mkoa wa Pwani.

“Vitu vilivyokamatwa ni pamoja na pikipiki tatu, dawa za kulevya aina ya Heroin kete 14, bhangi puli 48 na kete 382, magodoro na milango miwili ya nyumba,”alisema Lutumo.

Alitaja vitu vingine kuwa ni madirisha matatu, nondo 35, vyerehani viwili, mitungi ya gesi miwili, milango ya kontena miwili, reli ya krasha nne na pombe ya moshi lita 93.