Polisi yatoa mafunzo madereva gari za utalii

JESHI la Poloso mkoani Arusha leo limeungana na wadau wengine ikiwemo Chuo cha Ufundi Arusha pamoja Chama cha Mawakala wa waongoza Utalii nchini (TATO), kutoa mafunzo kwa madereva wa magari ya watalii katika kuelekea msimu wa utalii.

Mkuu wa usalama barabarani mkoani humo, Zauda Mohamed wakati akifungua mafunzo hayo amesema jeshi hilo linatoa mafunzo hayo, ili kuhakikisha usalama wa watalii ambao wataongezeka kwa wingi mkoani humo kuelekea msimu huo ambao utaanza hivi karibuni.

Amesema mafunzo hayo yatawaongezea weledi madereva hao katika utendaji wao wa kazi, ambao utafanikisha watalii wote wanaofika mkoani humo kuwa salama wakiwa barabarani.

Pia amesema kupitia mafunzo hayo, madereva hao wataelekezwa namna bora ya kuwasiliana na Jeshi la Polisi ikiwa watapata changamoto za kiusalama wanapokuwa barabarani na wageni, ili jeshi hilo liweze kuzitatua kwa haraka.

Amewataka madereva hao kuhakikisha wanazingatia sheria za usalama barabarani, ili watumiaji wa barabara hususani wageni wanaotoka sehemu moja kwenda nyingine kuwa salama.

Mkuu wa Kituo cha Polisi Utalii na Diplomasia, Waziri Tenga amebainisha kuwa mafunzo hayo yameandaliwa kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kuutangaza utalii, ili kuongeza ujuzi na weledi kwa madereva hao katika kuhakikisha wanakua salama wanapokuwa na watalii barabarani.

Naye daktari Yusuph Mhando ambaye ni Makamu Mkuu wa chuo anayeshughulikia masuala ya Taaluma na Utafiti toka Chuo cha Ufundi Arusha, amesema chuo hicho kipo tayari na kimejipanga kuhakikisha wanatoa mafunzo bora kwa madereva hao, ili shughuli zao ziweze kufanyika kwa ufanisi zaidi.

Sirili Akko ambaye ni Katibu Mtendaji wa TATO, amesema waliomba mafunzo hayo kufanyika, ili kuwajengea uwezo madereva hao kabla ya kuanza msimu wa utalii hivi karibuni, ambapo wanatarajia kupokea idadi kubwa ya wageni.

 

Habari Zifananazo

Back to top button