Polisi yatoa taarifa kifo cha dereva wa Asas

JESHI la Polisi limeanza kuchunguza taarifa ya kifo cha cha dereva Martin Chacha Mwita wa kampuni ya Transfuel Logistics Ltd aliyefariki mjini Iringa wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.

Wakati uchunguzi huo ukiendelea jeshi hilo limetoa rai kwa wananchi kujiepusha na utoaji wa taarifa za uongo ambazo hazijathibitishwa na mamlaka yoyote kuhusu kifo cha dereva huyo ambaye taarifa za mitandaoni zimeihusisha kampuni hiyo na kampuni yake mama ya Asas kushirikiana na askari wa SUMA JKT kumuua kwa kipigo dereva huyo.

Akizungumza na wanahabari leo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi wa Polisi Mwandamizi (SACP), Allan Bukumbi alisema marehemu Chacha alilazwa katika hospitali hiyo akitokea Gereza Kuu la Mkoa wa Iringa alikokuwa amefungwa kwa miezi mitatu baada ya kupatikana na kosa la kuiba lita za disel 383 kutoka kwa mwajiri wake.

“Februari 28, 2024 Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa tulipokea taarifa kutoka kwa Mkuu wa Gereza la Iringa kuhusu kifo cha mfungwa namba 47/2024 aitwaye Martin Mwita Chacha mwenye umri wa miaka 46,” alisema.

Alisema dereva huyo mkazi wa Kunduchi Dar es Salaam alikuwa akitumikia kifungo hicho cha miezi mitatu toka Februari 20 mwaka huu baada ya kupatikana na hatia kwa kosa la jinai Namba 62/2024 la wizi wa mafuta lililotolewa hukumu na mahakama ya mwanzo Iringa Mjini.

“Taarifa za awali zinaonesha dereva huyo alipatwa na maumivu makali upande wa moyo na kulalamika kwa wafungwa wenzake waliokuwa nae kwenye shughuli za kilimo eneo la gereza la Mlolo na kukimbizwa hospitalini haraka,” alisema.

SACP Bukumbi alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Rufaa Mkoa wa Iringa kwa uchunguzi zaidi wa kitaalamu ili kubaini sababu ya kifo chake pamoja na kwamba taarifa za awali za daktari zinaonesha alikuwa na ugonjwa wa moyo.

“Ni hatari sana kwa watu wengine kutoa taarifa ambazo hazijafanyiwa uchunguzi wa kitaalamu na kuzisambaza. Hii inaweza kuwaingiza katika kosa la jinai kwa upande mmoja na kudaiwa kumlipa fidia mtu anayeweza kulalamika kuchafuliwa kwa upande mwingine,” alisema.

Kamanda Bukumbi alitoa rai kwa wananchi kujiepusha na utoaji wa taarifa za uongo na upotoshaji, kusimama kwenye ukweli na kuacha uzushi kwa malengo ya kuwachafua watu.

Habari Zifananazo

Back to top button