JESHI la Polisi kupitia kikosi cha kupambana na kuzuia wizi wa mifugo nchini, linawashikilia watuhumiwa 15, wanaodaiwa kuhusika katika tukio la mauaji ya wafugaji Kijiji cha Mbatamila, Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma.
Hayo yamesemwa leo Septemba 24, 2022 na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuia wizi wa Mifugo na Migogoro ya Wakulima na Wafugaji nchini, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Simon Pasua alipofika Kijiji cha Mbatamila.
Amesema Polisi inawashikilia watuhumiwa 15 kutokana na mauaji ya vijana wane wa familia moja katika kijiji hicho na kueleza kuwa wote waliofanya mauaji hayo, hawako salama na kuwataka wajisalimishe polisi.
Amewataka wakulima na wafugaji, kutojichukulia sheria mkononi, badala yake wafuate misingi ya sheria na taratibu katika kutatua changamoto zilizopo.
Pia amesema Polisi imekamata mifugo 159 iliyokuwa imeibwa Kijiji cha Mbatamila.