Pombe yaua mmoja, 53 walazwa

Pombe yaua mmoja, 53 walazwa

MTU mmoja amefariki dunia na wengine 53 wakiwemo watoto watatu wa Kijiji cha Nambala Kata ya Mlowo wilayani Mbozi wamelazwa hospitali mbalimbali kutokana na kunywa pombe ya kienyeji inayosadikika kuwa na sumu.

Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbozi, Keneth Lesilwa alisema wamepokea maiti ya Keneth Nzunda kutoka Hospitali ya Ilas inayomilikiwa na mtu binafsi na wagonjwa 45.

Alisema wagonjwa wengine sita wapo katika Hospitali ya Ilas na wawili katika Kituo cha Afya cha Sifika, hivyo idadi ya wagonjwa wote kufikia 54 waliofikishwa hospitalini.

Advertisement

Lesilwe alisema kati ya wagonjwa hao 54 kuna watoto watatu wenye umri chini ya miaka mitano ambao nao walinyweshwa pombe hiyo na wazazi pamoja na ndugu zao.

“Katika watoto hao, mmoja ana mwaka mmoja na miezi 11, mwingine ana miaka miwili na mwezi mmoja na mwingine ana miaka mitatu, hii inaonesha kuwa watoto wadogo wananyweshwa pombe,” alisema Lesilwa.

Alisema baada ya kupatiwa matibabu dalili za awali zinaonesha kuwa pombe waliyokunywa ilikuwa na sumu, ambapo wamechukua sampuli na kupelekwa kwa mkemia mkuu kwa ajili ya vipimo zaidi.

Dk Lesilwa alisema watu watano walitibiwa na kuruhusiwa na kudai kuwa waliolazwa hali zao zinaendelea vizuri, isipokuwa wanne ndio bado wanaendelea kupatiwa matibabu kwa ukaribu kutokana na wao kuendelea kutapika.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Ilas kilipotokea kifo kimoja, Dk Frederick Ngoi alisema waliwapokea wagonjwa saba wakiwa wanatapika mfululizo na kuharisha.

Alisema mgonjwa mmoja, Nzunda alifariki muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini hapo wakati akiendelea kupatia matibabu.

“Kati ya wagonjwa hao sita, watano ni wa familia moja ya Keneth Nzunda aliyefariki dunia,” alisema.

Wagonjwa sita waliobaki alisema wanaendelea na matibabu na hali zao zinaendelea kuimarika baada ya kuacha kutapika na kuharisha.

Akizungumza jana na HabariLEO, Kamanda wa Polisi mkoani Songwe, Alex Mkama alisema juzi kwamba watu hao walikunywa pombe hiyo katika klabu cha pombe kwenye Kijiji cha Nambala, Kata ya Mlowo wilayani Mbozi.

Alisema pombe hiyo ilitengenezwa na Siwema Mwampashe (40) na kwamba marehemu Kenneth Nzunda (57) alikuwa ndiye muuzaji wa pombe hiyo.

Wema Mwampashe aliyekoroga pombe hiyo na ambaye pia amelazwa kutokana na kunywa pombe hiyo alisema alianza kupata dalili za tumbo kuuma muda wa mchana na hatimaye kuanza kutapika na kuharisha.

Alisema baada ya kukoroga pombe yake waliinunua na kuipeleka klabuni na nyingine kupelekwa katika msiba uliokuwa jirani na mpaka sasa hajui ni nini kilitokea kwa sababu ni mkorogaji wa pombe wa muda mrefu.

Naye Juliana Tuya akiwa amelazwa hospitalini hapo alisema walikunywa pombe hiyo wakiwa katika msiba uliokuwa jirani lakini jioni walianza kuumwa matumbo na kuanza kutapika na kuharisha.