SERIKALI imesema imeongeza kiwango cha posho ya kujikimu kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka Sh 8,500 hadi Sh 10,000 kwa siku.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema hayo leo April 05,2023 bungeni jijini Dodoma wakati akisoma hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024.
“Mafanikio haya ni kielelezo tosha cha umakini, uzalendo, maono na mapenzi makubwa ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha ustawi wa maisha ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu”. Amesema Majaliwa.
Amesema kupitia Samia Scholarship, Serikali imetoa ufadhili kwa wanafunzi 244 wa kike wenye ufaulu wa juu ili kusoma katika vyuo vikuu mbalimbali katika fani za utabibu, uhandisi, sayansi, teknolojia na hisabati.
“Serikali imeendelea pia kutoa mikopo na kuongeza wigo wa upatikaji wa mikopo ya elimu ya juu sambamba na kuboresha miundombinu ya vyuo vya elimu ya juu nchini, katika mwaka 2022/2023, kiasi cha shilingi bilioni 654 zilitengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ikilinganishwa na shilingi bilioni 570 zilizotengwa mwaka 2021/2022, idadi ya wanufaika imeongezeka kutoka 177,605 mwaka 2021/2022 hadi 202,877 mwaka 2022/2023”.ameongeza Majaliwa.