PPRA Burundi yachota maarifa Tanzania

MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma Burundi (PPRA) imefanikiwa kuchota maarifa ya matumizi ya mfumo mpya wa manunuzi wa kielekroniki wa Tanzania (NeST) katika maandalizi yake ya kuachana na taratibu za manunuzi za jadi zinazotumia karatasi.

Mamlaka hiyo imepata maarifa hayo katika mafunzo ya wiki moja yaliyofanywa na PPRA Tanzania katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa, mjini Iringa.

Mfumo huo wa NeST kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa PPRA Tanzania, Eliakim Maswi una uwezo mkubwa wa kudhibiti rushwa, mchakato wa zabuni kuchelewa na kuongeza uwazi na ufanisi wa zabuni katika manunuzi ya sekta ya umma.

“Tunawashukuru sana watanzania kwa kutopokea na kutupa fursa ya kujifunza kuhusu mfumo wa manunuzi wa kielektroniki. Mafunzo haya ni sehemu ya maandalizi yetu ya kutoka kwenye mfumo wa zamani na kuingia katika matumizi ya mfumo wa kidigitali,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa PPRABurundi, Jean-Claude Nduwimana.

Nduwimana alisema mafunzo hayo ni muhimu sana kwao kwa kuzingatia kwamba tayari nchi yao imeanza kuunda mfumo mpya wa manunuzi utakaotumia mfumo wa kielektroniki kaama ilivyo Tanzania.

“Tunatarajia mfumo huu utaongeza uwazi katika ununuzi wa umma, usimamizi mzuri wa fedha za umma, kudhibiti vitendo vya rushwa, ufuatiliaji kukidhi sheria, uwajibikaji na udhibiti wa manunuzi,” alisema.

Hata hivyo alisema ili matumizi ya mfumo huo mpya yaweze kufanikiwa kuna haja ya kufanya mabadiliko ya sheria ya manunuzi na kuimarisha mtandao wa intaneti ambao upatikanaji wake ni chini ya asilimia 60.

“PPRA Burundi inaamini kuwa mfumo huu mpya utaleta maboresho na faida kubwa kwa sekta ya ununuzi wa umma na tuna imani kwamba utaimarisha uzoefu wa jumla wa ununuzi na kuongeza uwazi kwa asilimia 100,” alisema Mtaalamu wa Ufundi wa PPRA Burudi, Jean-Claude Nshimirimana.

Akibashiri kujitokeza kwa watu watakaoupinga mfumo huo kwasababu utadhibiti mianya ya upotevu wa fedha za umma, Nshimirimana aliwasihi wana Burundi kuwa tayari kwa mabadiliko hayo aliyosema yataimarisha mfumo wa manunuzi nchini humo na kuleta tija na ufanisi unaostahili.

“Rais wetu ameshatangaza kushirikiana na kampuni za ndani na nje kuboresha upatikanaji wa Intaneti na ili kuufanya mfumo huo mpya ufanikiwe angalau tunahitaji asilimia 85 ya Burundi nzima ifikiwemo na mtandao wa intaneti,” alisema.

Akizungumzia mafanikio ya mfumo huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa PPRA Tanzania alisema; “Mfumo huu wa kielektroniki tulianza kuujenga Julai 2022 na kuanza kuutumia ilipofika Julai 1, 2023.”

Maswi alisema toka uanze kufanya kazi, tayari taasisi 1117 zimesajiliwa huku taasisi 980 kati yake zimekwishaweka mipango yao ya ununuzi kwa kutumia mfumo huo.

Kwa kupitia mafanikio hayo aliipongeza halmashauri ya Kwimba akisema imetumia mfumo huo kutangaza tenda 404 ikifuatiwa na halmashauri ya wilaya ya Ngara iliyotangaza tenda 321 katika kipindi cha mwaka mmoja tu wa mfumo huo.

“Nia yetu ni kuhakikisha tunaongeza uwazi katika ununuzi wa umma na tunaamini na wenzetu wa Burundi watatumia mfumo huo na kupata mafanikio haya. Tunamshukuru Rais kwa kutuwezesha kufanya haya ili manunuzi ya serikali yanaendana na mipango tuliyokubaliana,” alisema.

Aliwakumbusha wafanyabiashara wote kuomba zabuni kwa kutumia mfumo huo mpya kama wanataka kupata kazi za serikali.

Habari Zifananazo

Back to top button