Presha ya macho kiini cha upofu

Wenye umri wa miaka 40 hatarinii

DAR ES SALAAM: Wakati dunia inaadhimisha wiki ya presha ya macho, ugonjwa huo umetajwa kuwa sababu kuu ya upofu usiotibika duniani.

Akizungumza leo Machi 14, 2024 katika kituo cha mabasi cha Magufuli ambapo CCBRT imeweka kambi maalum ya kuwapima macho bure, madereva, abiria, mama lishe, na wabeba mizigo katika kituo hicho, Daktari Bingwa wa macho kutoka Hospitali ya CCBRT, Simson Ching’anga amesema presha ya macho hutokea pale ambapo mshipa wa fahamu unaopeleka mawasiliano kwenye ubongo kushambuliwa   kutokana na presha kali.

Amesema ugonjwa huo wa presha ya macho unazuilika na usipotibiwa haraka unasababisha upofu.

“Ugonjwa huo utokea pale ambapo presha ya macho inazidi kiwango chake, kiwango cha presha ya macho ni 10 mpaka 21 milimita kinapokuwa zaidi kinaharibu mishipa ya fahamu,”amesema Ching’anga na kuongeza

“Mshipa huu wa fahamu ndio unaopeleka taarifa kwenye ubongo kutafsiri vitu tunavyoviona, inapotokea changamoto ya mshipa huo, kuathiriwa na presha, mshipa unaharibika na kusababisha mtu kuwa kipofu,”amesema

Aidha, amesema watu waliopo hatarini kupata presha ya macho ni wenye umri wa kuanzia miaka 40 na kuendelea na kuwashauri kuwa na desturi ya kufanya uchunguzi wa mara kwa mara ili kubaini kama viashiria vya presha ya macho vimeanza au la na kwamba iwapo akibainika mapema tatizo hilo linatibika na kuepusha upofu.

“Ugonjwa huu hauna dalili za moja kwa moja, hatua za awali mtu sio rahisi kubaini kuwa na presha ya macho, wengi tunawapokea wameshaathirika kwa kiwango kikubwa na kukosa kuona,”amesema

Hata hivyo, Ching’anga , anasema dalili za kwanza ambayo mgonjwa anaweza kuiona ni kupoteza uwezo wa kuona na hii ni hatua za juu kabisa.

Amesema, baadhi ya wagonjwa wachache wanaweza pata dalili kama, kuona rangi za upinde wa mvua unapoangalia taa, kupoteza uoni kabisa, uoni hafifu, kupungua uwezo wa kuona kwa pembeni, na maumivu ya kichwa.
Anasema kuwa watu wenye umri kuanzia miaka 40 na kuendelea wako katika hatari ya kupata ugonjwa huu, kama ilivyo kwa wale ambao wazazi wao au ndugu zao wa kuzaliwa wamewahi kuwa na ugonjwa wa presha ya macho.

Amesema, mtu unaweza kujikinga na ugonjwa huo kwa kufanya uchunguzi wa afya ya macho mara kwa mara na kama kwenu kuna historia ya ugonjwa wa presha ya macho, wanafamilia wafanye uchunguzi wa macho mapema, kama mtoto anafikicha sana macho yake yanatoa machozi na kuonekana kuwa makubwa apelekwe kwenye kituo cha afya au hospitali iliyoko karibu kwa ajili ya uchunguzi na akashauri matumizi mazuri ya dawa za macho kadri mtu anavyoshauriwa na daktari.

Dk. Ching’anga anasema utaratibu wa upimaji wa macho ufanywe kila baada ya miaka miwili ikiwa uko chini ya umri wa miaka 40, kwa wale wenye umri 40 hadi 64 wafanye uchunguzi wa macho yao kila mwaka, na umri zaidi ya miaka 64 wafanye hivyo kila baada ya miezi sita.

Kuhusu matibabu daktari huyo bingwa wa macho CCBRT anasema presha ya macho hutibiwa kwa vidonge vya kumeza, dawa ya matone kudondoshea kwenye macho, upasuaji, matibabu kwa njia ya kipandikizi na mionzi.

Nae, Dakari wa macho kutoka Idara ya Macho Polisi Barracks ( Kilwa Road), Erick Rafael ametoa wito kwa madereva na wasafiri kupima presha ya macho bure ili watambue afya zao.

“Ugonjwa wa presha ya macho hauna  dalili za moja kwa moja, ni vema watu wakapima mara kwa mara angalau kila baada ya miezi sita kuepuka upofu,”amesema.

Kwa upande wa Meneja Habari wa hospitali ya CCBRT Abdul Kajumulo amesema kuwa kambi  hiyo maalum ya upimaji macho bure ni muendelezo wa kampeni zinazofanywa na hospitali ya CCBRT Kwa kusirikiana na wadau wake lengo ni kuwafikia watu wengi wenye uhitaji.

Zoezi hilo la upiamaji wa afya ya macho limeambatana pia na upimaji wa bure wa magonjwa mbalimbali ya figo, presha, sukari na uchangiaji damu.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2019 inaonyesha watu bilioni 2.2 duniani kote wana uoni hafifu au upofu, kutokana na ukosefu wa huduma bora za afya.

Habari Zifananazo

Back to top button