Prof Mkenda atangaza vipaumbele 5 elimu  

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetaja vipaumbele vitano itakavyovitekeleza katika mwaka wa fedha 2023/24 ili kuongeza ubora wa elimu na kuwezesha vijana kupata maarifa.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ametaja kipaumbele kimojawapo ni kukamilisha mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na mitaala ya elimu na kuanza utekelezaji wake.

Profesa Mkenda alisema hayo bungeni Dodoma jana wakati anawasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Alitaja kipaumbele kingine ni kuongeza fursa na ubora wa mafunzo ya ufundi katika elimu ya sekondari na vyuo vya Kati vya ufundi, kuongeza fursa na ubora wa elimu ya msingi na sekondari, kuongeza fursa na ubora wa elimu ya juu na kuimarisha uwezo wa nchi katika utafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Pia Profesa Mkenda alisema serikali itafanya mapitio na marekebisho ya sheria ya elimu kwa kuzingatia maelekezo ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 na sheria za taasisi za elimu ili iendane na mahitaji ya toleo jipya la sera na mitaala na itaandaa mwongozo wa chakula na lishe.

Alisema serikali itawezesha ukarabati shule za sekondari za ufundi na kuzipatia vifaa vya kujifunzia na kufundishia huku ikiboresha vyuo vya ualimu 10 na kujenga karakana 10 na kuweka mitambo na vifaa katika vyuo vya ualimu.

“Serikali itasajili vyuo 130 vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi na hivyo kuwa na jumla ya vyuo 485 vya elimu ya ufundi na vyuo 973 vya mafunzo ya ufundi stadi ambavyo vitaongeza idadi ya wanachuo kutoka 380,748 hadi kufikia 680, 000,” alisema Profesa Mkenda.

Alisema itaongeza udahili wa wanafunzi katika vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi kutoka 51,382 hadi 66,459 wakiwemo 5,000 kutoka kwenye mazingira magumu; 1,500 wenye mahitaji maalumu na wajasiriamali 2,000 watakaopatiwa mafunzo kupitia programu ya INTEP na itadahili wanafunzi 660 katika Chuo cha Ualimu wa Mafunzo ya Ufundi Stadi Morogoro – MVTTC kwa lengo la kuongeza idadi ya walimu wanaofundisha katika Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Vyuo vya Ualimu wa Mafunzo ya Ufundi.

Pia Profesa Mkenda itafanya ufuatiliaji, uthibiti na tathmini kwa vyuo 400 vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi na kuhakiki mitaala 230 ya vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ili kuthibiti ubora wa elimu na mafunzo na itahakiki udahili wa wanafunzi 250,000 wa vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.

“Serikali itaongeza idadi ya walimu wa amali katika taasisi za umma kutoka 788 hadi 900 ili kukidhi mahitaji ya walimu wa masomo ya ufundi,” alisema.

Alisema serikali itaendelea kutekeleza programu ya uimarishaji wa ujuzi katika kampuni 12, itatoa mafunzo kwa wanagenzi 18,000 kutoka sekta isiyo rasmi na kuwezesha mafunzo ya uanagenzi katika vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi vya mikoa minne.

Profesa Mkenda alisema serikali itasajili shule za msingi na sekondari takribani 560 ambapo awali pekee 20, awali na msingi 380 (serikali 250 na zisizo za serikali 130), sekondari 165 (serikali 135 na zisizo za serikali 30), chuo cha ualimu kimoja cha binafsi na nyingine kwa kuzingatia maombi yatakayowasilishwa na kukidhi vigezo.

Pia itaanza kusajili shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu kwa mfumo wa kielektroniki kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuwafikia wadau wengi zaidi.

“Serikali itanunua na kusambaza zana na vifaa saidizi kwa wakufunzi, walimu na walimu tarajali wenye mahitaji maalumu ili kuimarisha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji wa elimu maalumu na itafanya ufuatiliaji na tathmini katika shule zinazopokea wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa lengo la kutoa ushauri wa kitaalamu,” alisema.

Alisema wizara itafanya tathmini ya jumla katika mafanikio ya wanafunzi; ubora wa ufundishaji kwa ujifunzaji na upimaji; ubora wa uongozi na utawala; ubora na mazingira ya shule na matokeo yake katika ustawi, afya na usalama wa wanafunzi na ushiriki wa jamii katika asasi takribani 6,700 (shule za awali na msingi 5,220, sekondari 1,422; na vyuo vya ualimu 58) kwa lengo la kutoa ushauri na mapendekezo kwa ajili ya kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.

“Itafanya tathmini ya ufuatiliaji katika asasi 1,280 (awali na msingi 1,021; sekondari 253; na vyuo vya ualimu 6) zilizopata matokeo yasioridhisha wakati wa tathmini ya jumla ili kubaini hali ya utekelezaji wa ushauri na mapendekezo yaliyotolewa katika tathmini ya jumla,” alisema.

Profesa Mkenda alisema wizara itafanya utafiti katika maeneo mawili ya tathmini ya upimaji wa elimu ya sekondari kidato cha pili ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji; na itafanya utafiti tatuzi katika maeneo ya kielimu katika shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu kwa ajili ya kubaini mafanikio na changamoto za utoaji wa elimu nchini na kutoa mapendekezo stahiki.

Alisema Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) itaanzisha kituo cha umahiri kitakachotekeleza kazi za ujasiriamali, ubunifu na uhawilishaji wa teknolojia kwa kubiasharisha ubunifu ikiwemo kubadilisha magari yanayotumia mafuta ya petroli kutumia gesi asilia na bajaji zinazotumia mafuta ya petroli kutumia umeme.

Habari Zifananazo

Back to top button