Prof. Mkenda atoa maelekezo huduma za maktaba

DAR ES SALAAM; WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.

Adolf Mkenda amesema ni tarafa nne peke yake zenye maktaba nchini na kuitaka Bodi ya Huduma za Maktaba kuliona hilo na kuhakikisha maktaba zinakuwepo maeneo mbalimbali.

Amesema hayo Dar es Salaam wakati akitoa wito kwa wakazi wa jimbo la Rombo mkoani Kilimanjaro waishio Dar es Salaam kukutana Mei 5,2024 eneo la Msimbazi ili kujadili masuala mbalimbali maendeleo.

Advertisement

Amesema siku za nyuma shule mbalimbali zilikuwa na maktaba lakini kwa sasa mwamko umepungua na kuielekeza bodi hiyo kuhakikisha kuwa bajeti yao isishuke na waende kila tarafa nchini kununua na kusambaza vitabu.

“Ninaiombia bodi wakimaliza marekebisho wanayofanya kwa sasa wajielekeza kwenye maktaba kusambaza vitabu, waangalie vyumba katika maneo ya misikiti, makanisa, na hata shule ili kuhakikisha maktaba zinakuwepo sehemu mbalimbali,” amesema.

Ametoa mfano kwa wakazi wa Kata ya Mraweni iliyopo wilaya ya Rombo kuwa wamejenga chumba cha maktaba wenyewe na sasa ameigiza bodi hiyo kupeleka vitabu .

Pia ametoa wito kwa watu binafsi na wenye mapenzi mema kuungana katika suala la kujenga maktaba katika maeneo mbalimbali nchini, ili kujenga utamaduni wa kusoma kwa mustakabali wa elimu nchini.

Kuhusu kukutana kwa wakazi wa Rombo amesema lengo ni kujadili kuhusu maendeleo ya jimbo hilo na kwamba wabunge na madiwani wote watakuwepo kutoa taarifa mbalimbali za maendeleo na kupokea mapendekezo pia.