Prof. Mkenda: Kuishia la sita haianzi mwakani

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema mchakato wa mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na Mabadiliko ya Mitaala umekamilika kwa ngazi ya utendaji na umewasilishwa ngazi ya maamuzi na kwamba hakuna mwanafunzi atakayeishia daras la sita kwa mwaka 2024 wala 2025.

Amesema mchakato huo ukifikia uamuzi utatekelezwa kwa umakini na kuwa wametafuta njia ya kati ili watu wasichoke na mageuzi.

“Watu wamekua wakiuliza uliza lakini si mwakani wala mwaka kesho kutwa, tutafanya mabadiliko kwa umakini mkubwa sana na tutaanza na wale ambao wataanza darasa la kwanza sio ambao tayari wapo shule.”Amesema Mkenda na kuongeza

“Niwaeleze umma wa Watanzania kwamba, hatusemi sasa ndio elimu yetu inakwenda hadi dasara la sita hapana, darasa la saba bado lipo, maamuzi yatakapofanyika itachukua muda kidogo kuingia elimu ya msingi ya darasa la sita, kwa sababu mapendekezo yaliyopo ni kuwa mitaala mipya itatekelezwa elimu ya awali, darasa la kwanza , la tatu alafu kidato cha kwanza, kidato cha tano na vyuo vya ualimu,”amesema.

Mkenda ameyasema hayo leo Agosti 11, 2023 katika hafla ya utiaji saini hati ya makubaliano baina ya Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), ya kushirikiana kuandaa vitabu vya kiada na ziada zitakavyosambazwa shuleni vinavyoelezea historia ya Tanzania na Ukombozi wa Bara la Afrika.

Amesema, mchakato wa mapitio hayo ya sera na mabadiliko ya mitaala umechukua muda mrefu kwa sababu ulikuwa shirikishi na wadau wote wamehusishwa.

“Watu walilalamika serikali inaongea tu haitekelezi, lakini nami nawakumbusha zamani walilalamika mabadiliko ya elimu yalifanywa ghafla kwa hivyo mapitio ya sasa wamewashirikisha watu wote na fursa ilitolewa na kutangazwa sana na tuliweka kwenye tovuti na walikuja,”amesema Mkenda.

Amesema tayari umekamilika na umewasilishwa ngazi ya maamuzi na yakitolewa umma utatangaziwa na kusema pamoja na kuwa mitaala ilikuwa inakwenda kiufundi, imefanywa kukiwa na mabadiliko makubwa ya sera ya elimu.

Aidha, amesema Sera ya Elimu inataka kutekelezwa kwa pendekezo lililotoka mwaka 2014 kwamba elimu ya msingi iwe miaka sita lakini elimu ya lazima iwe miaka 10 hjvyo haiwezekani kwenda na mitaala inayoakisi mabadiliko hayo, kabla ya mapitio ya sera yenyewe haijapita.

Habari Zifananazo

Back to top button