Prof. Pembe: Vijana wapatiwe elimu ya afya ya uzazi mapema

Kuepusha madhara ya utoaji mimba holela, sheria yaguswa

MHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na bingwa wa magonjwa  ya wanawake, Profesa Andrea Pembe amesema elimu ya afya ya uzazi ianze kutolewa mapema kwa vijana kuanzia miaka tisa hadi 12 kabla ya kujihusisha na vitendo vya kujamiana.

Profesa Pemba ameyasema hayo jijini Dar es Salaam katika Kongamano la wadau wa masuala ya Afya ya Uzazi lililoandaliwa na Chama cha Wanasheria Wanawake (Tawla).

Amesema, mimba zisizotarajiwa zinazuilika hivyo ni muhimu elimu ya masuala ya afya ya uzazi na kujitambua itolewe mapema ili kuzuia wimbi la mimba za utotoni na utoaji mimba usio salama,

“Elimu ya afya ya uzazi ianze kutolewa kabla ya watu hawajaanza tendo la ndoa, kutumia elimu hiyo ili kuepuka mimba za ujanani lakini pia ata wakipata mimba wanakuwa na taarifa sahihi na kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya zao wenyewe.”Amesema Profesa Pembe na kuongeza

“Siku hizi binti anavunja ungo akiwa na  miaka 11, 12 tofauti na zamani walikuwa wanavunja miaka 14, umri huo tayari wawe wameshapewa elimu ya kujitambua.”Amesisitiza

Amesema , binti anapovunja ungo hali ya kimwili inabadilika wanakuwa na hamu, lazima wafundishwe kujizuia matamanio yao.

Amesema elimu ya afya ya uzazi ni pana na ina vitu vingi watu wanatakiwa kuvifahamu.

Chanzo cha utoaji wa mimba

Profesa Pembe,  anasema jamii haijawa na uelewa wa kutosha kuhusiana na tatizo la utoaji wa mimba  hivyo jamii inahitaji elimu ya kutosha kukabiliana na hali hiyo huku umasikini nao ukitajwa kuwa ni chanzo cha utoaji mimba kwa njia isiyo salama.

Anasema mfumo dume pia umechangia wanawake wengi kutoa mimba kutokana na kukosa maelewano ndani ya ndoa na wakati mwingine kukosa uamuzi sahihi.

Aidha Profesa Pembe ameelezea madhara ambayo wanawake wanapata baada ya kubeba zisizotarajiwa na matokeo yake uishia kwenye utoaji usio salama.

Madhara ya utoaji mimba kiholela

Madhara ambayo mtu anayetoa mimba kiholela yupo hatarini kukumbana nayo ni kifo, ugumba au figo kushindwa kufanya kazi.

Profesa Pembe anasema Tanzania suala zima la utoaji mimba lipo juu kama nchi nyingine za Afrika Mashariki na Kati, wakina mama 36 kati ya 1,000 wanatoa mimba

 

“Sasa tukiangalia kwa ujumla wake utoaji mimba una madhara sana hasa kwa mama mwenyewe anaweza kupoteza damu nyingi, anaweza kuwa na tatizo la maambukizi makali ya bakteria yanayopelekea mwili na viungo kushindwa kufanya kazi na kupoteza uhai wake.

“Suala zima la mama kupata ugumba kutokana na mirija kuziba na hivyo ujauzito kutokufika katika nyumba ya uzazi.

“Ukuta ya mbele na nyuma wa mfuko wa uzazi kugandamana pamoja na kupoteza damu za hedhi na kushindwa kupata mimba hapo baadae.”Amesema

Figo Kushindwa kufanya Kazi

Daktari bingwa figo, kutoka hospitali ya Sekou Toure Mwanza Ezekiel Petro anasema utoaji mimba holela ni moja ya chanzo cha matatizo ya figo.

Anasema ni kwa sababu wengi wanatoa kwa njia zisizo salama ikiwemo za kienyeji na ufanyika vichochoroni.

“Mimba nyingi ufanyika vichochoroni pasipo na wataalam wa masuala ya uzazi kusimamia mchakato kutokana na sheria za nchi kutoruhusu utoaji mimba,” anasema na kuongeza

“Matokeo yake baada ya mimba kuharibiwa, mhusika  anaweza kutokwa damu nyingi, lakini isiyoonekana kwa macho, kwani inakimbilia na kujificha katika mfuko wa uzazi na hivyo kuathiri figo.

“Haya ni matatizo yanayoweza pia kumkumba mjamzito baada ya kujifungua,” anasema

Asilimia 7 ya Watanzania wanaugua figo

Amefafanua kwamba damu ikitoka nyingi na kukimbilia kwenye mfuko wa uzazi maana yake figo inakosa damu ya kutosha kwa ajili ya kazi yake ya kuchuja taka mwili na kuzitoa nje.na hivyo kupelekea uharibifu.

Sheria inasemaje`

Mkurugenzi wa Uchechemuzi na Maboresho Fulgence Massawe kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) anasema kwa mujibu wa kifungu 150 hadi 152 cha Sheria ya Makosa ya Jinai  kinazuia utaoji mimba wa aina yoyote.

“Kwa mujibu wa sheria adhabu zipo za aina tatu ambazo ni kwanza, mtu ambaye atamsaidia mwenye mimba kutoa ujauzito huo, atahukumiwa kifungo kisichopungua miaka 14 jela, kwa mtu ambaye atatoa dawa au vifaa kwa ajili ya kutoa mimba adhabu yake ni kifungo cha miaka  mitatu jela na kwa upande wa mhusika mwenyewe kwa maana ya mwenye mimba akibainika kutoa ujauzito wake mwenyewe atahukumiwa kifungo cha miaka saba jela,” anafafanua  Masawe

Anasema, Sheria ya Makosa ya Jinai kifungu 230 kinaruhusu  utoaji wa mimba kwa ajili ya kuokoa maisha ya mama pekee endapo atapewa ruhusa kwa kibali maalumu cha daktari.

“Katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, sehemu ya tatu ibara 14 inaeleza bayana kuwa kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria,” anasema Masawe

 Nini kifanyike?

Wadau mbalimbali wa masuala ya afya, wamependekeza  Serikali itunge sheria mpya ambayo itasaidia suala la utoaji mimba liwe la kisheria ili vifo vinavyotokana na masuala ya uzazi vipungue.

Julius Titus Afisa wa Sheria kutoka Tawla anasema  nchi zilizoruhusiwa utoaji mimba kwa wanawake zina idadi ndogo ya vifo vinavyotokana na uzazi pia zina kiwango kidogo cha utoaji mimba  kwa njia salama kwa sababu jamii imepata elimu ya kutosha tofauti na nchi ambazo hazijaruhusu utaoji wa mimba, zimekuwa na idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na masuala ya uzazi.

“Ukibana sheria, unaruhusu utoaji mimba usio salama na ukiruhusu sheria hiyo vifo vinavyotokana na masuala ya uzazi vitapungua, kwani utoaji mimba kwa njia salama unamfanya mwanamke kuwa salama zaidi lakini kwa utoaji mimba usiofuata njia salama una muweka mwanamke katika hatari ya kupata magonjwa na pengine kifo,” anasema.

 

Habari Zifananazo

Back to top button