DAR ES SALAAM: Mratibu wa Tamasha la ZIFF Bara, Profesa Martin Mhando amesema filamu ni chombo kinachoweza kusaidia binadamu kujitambua mwenyewe na kutambua namna ya kuifanya dunia kuwa sehemu ya amani badala ya vita.
Profesa Mhando amesema filamu zinasaidia kumtambulisha binadamu lakini pia ni chombo ambacho kwa kawaida kinafanywa chepesi sana lakini kazi yake ni kubwa sana.
“Filamu zina faida kubwa na kwa upande wa diplomasia filamu ndiyo chombo kikubwa zaidi kuliko vyote kwasababu kwa kuonyesha mahusiano ya kimataifa katika filamu tunaweza kuonyesha namna gani amani ni kitu cha muhimu sana katika dunia,” ameeleza Profesa Mhando.
Profesa Mhando amesema binadamu wote wapo sawa ndiyo maana kupitia filamu tunaweza kujilinganisha na watu wa mataifa mengine kimaisha.