MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeipongeza serikali kwa kulipa madeni kwa mfuko huo ‘Hati Fungani’ ya Sh trilioni 2.17.
Meneja wa mfuko huo Kanda ya Mashariki inayojumuisha Mkoa wa Pwani na Morogoro, Zaida Mahava amesema hayo leo mjini Morogoro baada ya kufunguliwa mafunzo maalumu ya wastaafu watarajiwa wa PSSSF.
Alisema mafunzo hayo ya siku mbili yameshirikisha wastaafu watarajiwa 500 kutoka idara za serikali, serikali za mitaa na mashirika ya umma katika Mkoa wa Morogoro na kubeba kauli mbiu: “ Wekeza Mafao yako Sehemu Salama kwa Uhakika wa Ukwasi”.
Mahava alisema malipo hayo yameusaidia Mfuko wa PSSSF kuwa na uhakika na kufanya kazi wa kujiamini kwa sababu Mfuko una uwezo wa kulipa mafao ya wastaafu wakiwemo wa Kanda ya Mashariki anayoiongoza.
“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo inaunga mkono kwa kusaidia kwa kiwango kikubwa Mfuko wetu wa PSSSF” alisema Mahava.
Meneja wa Mfuko wa Kanda ya Mashariki alisema moja ya sababu iliyofanywa kwa kuunganishwa kwa mifuko ilikuwa ni kutokana na baadhi ya mifuko kutokuwa na uhakika wa kulipa mafao.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Paul Kijazi alisema mwaka wa fedha wa bajeti 2023/2024 watumishi wa umma 11,000 wanatarajia kustaafu kwa mujibu wa sheria.
Kijazi ambaye ni Meneja wa Rasilimali Watu wa Mfuko huo alisema idadi hiyo inaweza kuongezeka kutokana na wale ambao wanaoomba kustaafu utumishi wa umma kwa hiari wanapofikisha umri wa miaka 55.
Pamoja na hayo alisema kuwa Mfuko wa PSSSF kwa sasa inawahudumia wastaafu waliopo kwenye mfumo wa malipo ya kila mwezi wapatao 160,000.
Katika hatua nyingine Mfuko wa PSSSF umeanzisha mpango mkakati wa kuunga mkono serikali katika suala la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuweka lengo la mwaka huu kupanda miti milioni tano.
Kwenye mafunzo ya wastaafu watarajiwa hao walipatiwa miti ya matunda, kila mmoja alipewa miche miwili kwa ajili ya kwenda kuotesha baada ya kupatiwa elimu wataalamu wa kilimo kuhusu namna uoteshaji na utunzaji.