PSSSF waja kisasa zaidi mafao ya wastaafu

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF ,Hosea Kashimba akizungumza na mmoja wa wanachama wa mfuko huo waliotembelea banda hilo.

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma(PSSSF),Hosea Kashimba amesema mfuko huo utazindua mpango kutoa mafao kwa wastaafu wake kwa njia  ya mtandao  na mnufaika hatapaswa kufika ofisini kushughulikia mafao hayo.

Pia amesema wastaafu wote wa mfuko huo walio nje ya nchi wanaweza kufanya uhakiki wa taarifa zao kwa mfuko kwa kwenda katika ofisi za ubalozi katika nchi walizoko na kisha taarifa hizo zitatumwa na ubalozi kwenda PSSSF.

Ameyasema hayo katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, (DITF),yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba na kuratibiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania(TanTrade).

Advertisement

Akizungumza katika banda la PSSSF, Kashimba amesema ndani ya miezi miwili kuanzia sasa watazindua mpango huo kwa wastaafu watarajiwa ambao watajaziwa fomu zao mtandaoni, wakiwa eneo lake la kazi, kisha mwajiri ataifanyia kazi na kuituma kwa mfuko.

“Sisi tutaipata na kuifanyia kazi na tutatuma mafao moja kwa moja kwenye akaunti ya mwanachama wetu bila ya yeye kuja ofisini kwetu kufuatilia mafao yake,”amesema Kashimba.

Amesema PSSSF inachofanya sasa ni kujiandaa na watumishi wake wataanza kupita kwa waajiri kutoa mafunzo ya jinsi ya kutumia mfumo huo kabla ya kuanza kuutumia.

Kuhusu kazi ya uhakiki wa wastaafu walio nje ya nchi, Kashimba alisema wanaweza kuhakiki taarifa zao kwa  kutumia ofisi za Balozi za Tanzania kwenye mataifa waliyoko kwa wao kwenda na kutoa taarifa kisha zitatumwa moja kwa moja kwa PSSSF nchini.

Amesema mfuko wa PSSSF hadi sasa una jumla ya wanachama 780,000  na unakusanya michango kwa mwaka ya shilingi trilioni 1.65 na kwa mwezi unalipa mafao kwa wanachama wake ya shilingi bilioni 65 na hadi sasa wanufaika 160,000 wanalipwa kila mwezi.

Aidha kwa mwaka mfuko huo unalipa mafao ya shilingi trilioni 1.6

Kuhusu uwekezaji alisema mfuko umewekeza zaidi ya asilimia 60 kwenye hati fungani kwa thamani ya shilingi trilioni 4.6 na maeneo mengine ya uwekezaji ni majengo yaliyogharimu shilingi trilioni 1.1, viwanda vilivyogharimu shiilingi bilioni 169 na uwekezaji katika mabenki wa thamani ya shilingi bilioni 600.

”Tumewekeza kulinda thamani ya wanachama na hii imetuwezesha kulipa mafao kwa wakati,ndani ya siko 60 tunalipa mafao, hivyo wanachama wetu katika maonesho hayo tembeleeni banda lenu mpate taarifa mbalimbali za mfuko,”alisema Kashimba.

5 comments

Comments are closed.