Pugu Marathon kuanza Mei, 27, 2023

MBIO za Hisani za Pugu Marathon, zinatarajia kufanyika Mei 27, mwaka huu kuanzia eneo la Hija Pugu hadi Kisarawe.

Mbio hizo zitahusisha wanariadha katika kilometa 21, kilometa 10, mbio fupi kilometa tano na matembezi ya kilometa mbili.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Askofu wa Kanisa Katoliki wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, alisema wameanza maandalizi ya mbio hizo ambazo zitakuwa zikifanyika wiki ya mwisho ya kila mwaka.

Alisema lengo la mbio hizo ni kuchangisha fedha kwa ajili ya kuendeleza kituo cha Hija cha Pugu, kusaidia wagonjwa wenye uhitaji katika hospitali mbalimbali ikiwemo kukarabati nyumba aliyowahi kukaa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

“Tumeandaa mbio za Hisani za Pugu Marathon, ambazo zitakuwa zikifanyika kila mwaka, lengo ni kuchachisha fedha za kuendeleza kituo cha Hija cha Pugu, kutoa misaada kwa wagonjwa katika hospitali mbalimbali, kukarabati nyumba aliyowahi kuishi Baba wa Taifa, kudumisha afya na kujenga utamaduni wa kushiriki michezo,” alisema Askofu Ruwa’ichi.

Alisema kuwa anawaomba wanariadha mbalimbali kujitokeza kwa ajili ya kushiriki katika mbio hizo ambazo zitafanyika kwa mara ya kwanza mwaka huu na zitakuwa na mwendelezo kila mwaka.

Naye Katibu wa Kamati ya Mbio hizo, Marceline Nkwere, alisema wanawaomba wadau mbalimbali na makampuni kujitokeza kwa ajili ya kuwapa udhamini ili kuhakikisha wanafikia malengo waliyojiwekea.

Alisema wanaamini mbio hizo zitafanyika kwa ushindani zaidi kutokana na maandalizi wanayoyafanya.

Alisema washindi wa mbio hizo wanatarajiwa kupatiwa zawadi mbalimbali ambazo zitatangazwa baadaye pamoja na medali.

“Maandalizi yanakwenda vizuri na kwamba tunaomba wadau mbalimbali wajitokeze kutupatia udhamini ili kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea,” alisema.

Aliongeza usajili utakuwa ukifanyika kwa njia ya mtandao ambapo washiriki wa mbio za kilometa 21 na kilometa 10 watalipia sh. 30, 000, kilometa tano na mbili kiingilio ni sh. 20,000.

Habari Zifananazo

Back to top button