SERIKALI ya Urusi imeonesha imani kubwa kwa wananchi wake kutokana na utulivu waliouonesha wakati wa tishio la uasi la askari wa kundi la Wagner lililozua taharuki ya muda mfupi kabla mambo hayajawekwa sawa na hali ya utulivu kurejea.
Taarifa iliyotolewa na mamlaka nchini humo zinaeleza kuwa Rais Vladimir Putin alisema hakuwa na shaka ya kuungwa mkono na raia wa Urusi wakati wa kipindi kifupi cha uasi wa Wegner.
Ikulu ya Urusi imeendelea kusisitiza uwezo wa kimamlaka alio nao Putin wakijaribu kuonesha umoja wa kiserikali na kijeshi.
Juni 23, 2023 askari wa kundi la Wagner linalofanya kazi na jeshi la serikali ya nchi hiyo lilifanya uasi dhidi ya serikali jambo ambalo linaelezwa kusababishwa na mgogoro uliopo baina ya Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Sergei Shoigu na kiongozi wa kundi la Wagner, Yevgeny Prigozhin.
Ilieleza kuwa kitendo hicho cha Wagner kilikuwa ni ishara ya Prighozin kujibu mapigo ya madai ya kushambuliwa kwa vikosi vyake na majeshi ya Urusi.