Puto la kupunguza uzito linavyopunguza magonjwa yasiyoambukiza

MAGONJWA yasiyoambukiza (NCDs) ni yasiyoenea kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.

Hivi sasa NCDs imekuwa mzigo kwa taifa kutokana na kutumia gharama kubwa ya matibabu kwa muda mrefu na kupoteza nguvu kazi.

Wizara ya Afya imesema unene uliokithiri na uzito kupita kiasi ni kisababishi cha magonjwa yasiyoambukiza kwa asilimia 73 ya magonjwa hayo.

Imetaja vichocheo vingine ni changamoto za lishe zinazosababisha magonjwa hayo kwa asilimia 32 na matumizi ya tumbaku kwa asilimia 14.8.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2016, zinaonesha kuwa vifo milioni 42 sawa na asilimia 71 vilivyotokea duniani vilitokana na magonjwa hayo na asilimia 25 ya vifo hivyo viliwahusu wenye umri wa miaka 30 hadi 70.

Mkurugenzi wa Magonjwa Yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Dk James Kiologwe, anasema mzigo wa magonjwa umeongezeka nchini na vihatarishi vimeongezeka kwa kasi hivyo wanatakiwa kuangalia nini cha kufanya kudhibiti.

“Sasa watu wanaofanya ngono isiyo salama ni wachache kuliko wenye uzito kupindukia, mzigo unaongezeka, theluthi mbili hawajifahamu, wengine wanafika hospitali wakiwa na madhara zaidi,” anasema Dk Kiologwe.

Anasema tafiti zinaonesha kuwa kwa miaka 10 visababishi vimeongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza kuliko yanayoambukiza.

Dk Kiologwe anasema vihatarishi vinavyosababishwa na lishe isiyo sahihi ni asilimia 18 na vya matumizi ya pombe ni asilimia 15.9.

“Tumeona kuna haja ya kupata elimu kwa magonjwa yasiyoambukiza, tumeamua kutumia mhimili wa habari ili kutoa elimu sahihi na katika mapambano haya tunakinzana na changamoto za kibiashara na viwanda ambazo nao ni muhimu kupata elimu sahihi,” anasema Dk Kiologwe.

Anasema wanatengeneza timu kwa kila mkoa ili kutoa elimu ya magonjwa yasiyoambukiza na wanatarajia kuandaa tuzo kwa wanaoandika habari zinazohusu magonjwa hayo.

Anasema tabia bwete, ulaji usiofaa na kutokufanya mazoezi ni vyanzo vikubwa vya magonjwa hayo.

HUDUMA YA KUPUNGUZA UZITO YATOLEWA

Katika kudhibiti magonjwa hayo, kwa mara ya kwanza nchini, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili-Mloganzila jijini Dar es Salaam imeanza kutoa huduma ya kupunguza uzito uliokithiri kwa kuweka puto tumboni.

Hadi sasa watu 26 wenye uzito zaidi ya kilogramu 100 wamepata huduma hiyo inayogharimu Sh milioni 3.5 hadi milioni nne.

Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Mohammed Janabi anasema hawatoi huduma hiyo kwa sababu ya urembo bali wanalenga kusaidia watu.

“Hii ni operesheni yetu ya tatu leo na leo (Desemba 21, 2022) tumewafanyia watu wawili wote ni kilogramu 100 kwenda juu wa kwanza kilo 160 na wengine kilo 105, hawajafanya kwa sababu ya urembo. Wiki moja iliyopita tulifungua kliniki ya mafuta tunawakaribisha hospitali zingine zilete wagonjwa kupata huduma,” anasisitiza Profesa Janabi.

JINSI UNAVYOFANYIKA

Profesa Janabi anasema utoaji huduma hiyo utahusisha uingizaji wa mrija wa puto kupitia mdomo hali itakayopunguza kiwango cha chakula kwa mhusika.

“Tutaweka kwa miezi nane, tutaingiza kupitia mdomo hadi kwenye tumbo, hakuna upasuaji tunatumia mitambo ifike mahali pake tunajaza dawa, linapunguza ukubwa wa tumbo ukila kidogo utashiba hivyo tunategemea uzito utapungua.”

HUKINGA NA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA

Profesa Janabi anaeleza kuwa faida kubwa ni kusaidia kinga dhidi ya magonjwa ya kisukari, kiharusi, moyo na kushindwa kupumua.

Anabainisha kuwa matibabu yatakayotolewa ni siri ya mgonjwa ambapo pia matibabu hayo huchukua siku mbili tu.

“Siku ya kwanza unaweza kusikia kama una vidonda vya tumbo lakini baada ya muda utaendelea kawaida, hospitali hatukaribishi watu lakini tunawaomba wale wenye uzito mkubwa wafike kliniki tuna kliniki ya siku mbili hapa Mloganzila na siku mbili Muhimbili-Upanga,” anasisitiza.

Pamoja na hayo anasema pindi mgonjwa anapopatiwa huduma hiyo na kupungua atapata usaidizi wa mtaalamu wa lishe ili asiongeze tena kiwango cha kula na uzito kuongezeka tena.

“Kabla ya kumhudumia tutapima vitu vingine vyote ndio upate huduma, faida kubwa ni kitu ambacho baada ya miezi nane tutatoa na hali ya kula kidogo itaendelea na akirudi tabia ya mwanzo anaweza kuwekewa mara nyingine hivyo ni vyema kuweka kiasi.

“Na matatizo mengine ni ya kurithi ukiwa na mtoto ana uzito mkubwa mlete wakati mwingine unaweza kukuta mtoto amezaliwa na kilo nne watu wakaona ni kitu sahihi kumbe si kweli,” anasema Profesa Janabi.

Anasema gharama ya huduma hiyo nje ya nchi inategemea na nchi; India ni Sh milioni 15 hadi 20 na Ulaya ni Sh milioni 30 kwenda juu lakini nchini ni Sh milioni 3.5 hadi Sh milioni nne.

“Hii ni sehemu ya utalii tiba hivyo nchi za jirani tunatoa huduma hizi waje kupata huduma, ni tiba salama kama tunavyopandikiza figo, uloto na zingine wakitaka kupata huduma hapa ni rahisi,” anaeleza Profesa Janabi.

UZITO HUPUNGUA HARAKA

 Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji, Erick Kimaro anasema wanatarajia mtu kupungua kilogramu 30 na kuendelea kwa muda wa miezi nane.

Dk Kimaro anasema kama baluni ikipasuka katika baluni wameweka maji dawa hivyo maji yataonekana kwenye haja na itatolewa na kuwekwa nyingine.

“Tutapima magonjwa mengine mfano wenye shinikizo la damu tukipunguza uzito itawasaidia hivyo ni sehemu ya tiba.

WAJIPANGA KUTOA HUDUMA

Naibu Mkurugenzi wa Mloganzila, Dk Julieth Magandi anasema wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa wakati.

“Huduma hii inahusika na kuweka puto tumboni bila upasuaji kwa wagonjwa ambao wana uzito uliopitiliza kiwango kinachotakiwa na tumejipanga kuanzisha huduma hii katika mifumo miwili; wa kwanza tumeanzisha kliniki maalumu wagonjwa wote lazima wapime kiwango cha mafuta katika damu na kwa wale ambao wanataka kupunguza uzito wataonana na timu ya wataalamu kuhudumiwa,” anaeleza Dk Magandi.

Anasema mgonjwa anapofika moja kwa moja anapelekwa chumba maalumu na wataalamu wote wanaotakiwa watamwona na huduma atapewa akiwa sehemu moja.

Aidha, anabainisha kuwa tangu wameanza mwitikio umekuwa mkubwa na kusababisha kuanzisha kambi maalumu.

“Tukumbuke watu walikuwa wanasafiri kwenda nje lakini sasa huduma ipo ndani, wataalamu wapo wakutosha na vifaa vipo mgonjwa akija asubuhi jioni anatoka,” anasema.

UTALII WA MATIBABU

Mjumbe wa Medical Tourism Taifa, Abdulmalick Mollel, anaeleza kuwa wamekuwa wakirekodi vipande vya video na kutafsiri kwa lugha mbalimbali ili kutangaza huduma hiyo.

“Kwanza madaktari bingwa tayari tulishakaa nao na kuangalia maswali yanayohitaji katika jamii, wanapokuwa wamehojiwa tunakata vipande na kutafsiri kwa lugha mbalimbali na kutangaza huduma zinazopatikana na tumeshafanya hivyo na madaktari wapo wanajibu maswali kuhusu huduma hiyo.

“Na watu wanapigiwa simu kuelimishwa na pia hata baada ya kupata huduma wanatafutwa kujua hali zao zinaendeleaje,” anasema Mollel.

Daktari Bingwa wa Upasuaji, Kimaro alisema watu kutoka nchi mbalimbali wamekuwa wakitafuta huduma hiyo huku wengine tayari wameshafika kuipata.

“Nimepokea simu kutoka nchi mbalimbali kupata huduma za baluni kutoka Congo (DRC) wanataka huduma na Kenya na mwingine wa Syria amewekewa, tumepata simu nyingi na watu wanatafuta huduma na leo (Januari 20, mwaka huu) tunawafanyia watu sita,” anaeleza Dk Kimaro.

Habari Zifananazo

Back to top button