Raia 2643 DRC waomba hifadhi Kigoma
RAIA 2643 wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), wameingia mkoani Kigoma katika makundi makubwa wakiomba hifadhi ya ukimbizi wakieleza kukimbia mapigano nchini mwao.
Mkurugenzi wa Idara ya wakimbizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Sudi Mwakibasi, akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mjini Kigoma leo, amesema kuwa waomba hifadhi hao walianza kuingia nchini kuanzia Machi tano mwaka huu.
Mwakibasi alisema kuwa walipoanza kuingia nchini waomba hifadhi hao walikuwa kwenye makundi madogo, lakini ilipofika Machi 10 makundi makubwa ya watu 300 hadi 600 yalianza kuingia na kufika kwenye ofisi za idara ya wakimbizi na ofisi za Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR).
Mkurugenzi huyo wa idara ya wakimbizi alisema kuwa baada ya kuwapokea hapa mjini na kufanyiwa mahojiano, waomba hifadhi hao wanapelekwa kwenye kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu wilayani Kasulu wakisubiri mchakato wa maombi yao utakaofanywa na Tume ya Taifa ya kutoa haki ya ukimbizi kwa raia wa kigeni (NEC).
Akizungumzia ujio wa raia hao wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Mratibu wa idara ya wakimbizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi kanda ya Magharibi, Nashon Makundi, alisema kuwa sehemu kubwa ya waomba hifadhi hao waliingia nchini na kujibanza kwenye vijiji na wengine kuingia kinyemela kwenye kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu.
Hata hivyo alisema kuwa baadaye ili kuhalalisha ukaaji wao nchini na kuondoa kujificha wameamua kuripoti ofisi za MHA na ofisi za UNHCR, ambapo kwa sasa mchakato wa kuwapa hifadhi na misaada ya kibinadamu inaendelea wakati mchakato wa mahojiano kuthibitisha kama wanayo hadhi ya kupewa hadhi ya ukimbizi utafanyika.
Naye Mkuu wa Mkoa Kigoma,Thobias Andengenye akizungumza na wakimbizi hao katika hosteli ya Santa Martha Nzimano mjini Kigoma, aliwataka kutulia na kusubiri mchakato wa kuwapokea na kuwapa hifadhi unaosimamiwa na Idara ya wakimbizi na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhifadhi wakimbizi.
Baadhi ya waomba hifadhi walioingia nchini ambao kwa sasa wanahifadhiwa kwenye kituo cha muda cha Santa Martha Nzimano mjini Kigoma, walisema kuwa wamelazimika kukimbia nchini mwao na kuja Tanzania kutokana na kuongezeka kwa hali mbaya ya usalama ambao unahatarisha maisha yao.
Mmoja wa wakimbizi hao,Stanley Goliath anayetoka jimbo la Kivu ya Kaskazini alisema kuwa kwa siku za karibuni mapambano baina ya kundi la waasi la M23 na majeshi ya serikali yamekuwa makubwa na kuathiri maisha ya wananchi hivyo kulazimika kukimbia kunusuru maisha yake.