Raia wa Burundi akamatwa na AK47 Chato

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo

JESHI la Polisi mkoani Geita linamushikilia raia wa Burundi kwa tuhuma za kuingia nchini kinyume cha sheria pamoja na kumiliki silaha aina ya AK47 ambayo imekuwa ikitumika katika matukio ya uharifu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo ametoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari na kueleza raia huyo ametiwa mbaroni baada ya silaha hiyo kutumika kwenye mauaji ya mchimbaji mdogo Tegemeo Rashid (38) Novemba 2, 2022. Rashidi aliuwawa kwa kukatwa na kitu chenye makali shingoni na kichwani kijijini Ihanga, Kata ya Buziku wilayani Chato.

“Wakati wa utekelezaji wa mauaji hayo, wauaji walikuwa na silaha aina ya AK47 ambayo waliitumia kumutishia marehemu asimame wakati akiendesha pikipiki na ndipo walifanikiwa kumkamata.

Advertisement

“Kisha walimufunga kwa kamba ya katani shingoni na kumzungushia tumboni na mikononi na kumbuluza hadi umbali wa mita 170 toka eneo walipomusimamisha na kufanikisha adhima yao.

“Wakati wa kutekeleza mauaji hayo, alijitokeza msamalia mwema akitaka kumuokoa marehemu ndipo majambazi hao kwa kutumia silaha hiyo walifyatua risasi hewani ili kumtisha ashindwe kutoa msaada.”

Amesema jeshi la polisi limefuatilia na kufanikiwa kuwakamata watu wanne wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji hayo ambao wamekiri kuhusika na kisha kumtaja mmiliki wa AK47 kuwa ni raia wa Burundi.

“Juhudi zilifanyika na hatimaye jana usiku (Novemba 4) tulifanikiwa kumkamata huyo mrundi, lakini katika mahojiano aliweza kutuonyesha silaha aina ya AK47, ambayo haina namba za usajili ikiwa na risasi 11.

“Lakini pia amekiri kwamba anatokea Burundi na wenyeji wake ni watuhumiwa ambao walimpokea hapa kwetu kutuonyesha Bunduki hiyo ambayo alikuwa ameificha kwenye shamba la mahindi katika kijiji cha Buziku.” Ameeleza Kamanda.

Kamanda Jongo amesema jeshi la polisi linaendelea kukamilisha hatua za kisheria ili kuwafikisha mahakmani watuhumiwa hao.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *