RAIA 22 kutoka Burundi na Uganda wameokolewa kutoka katika mashirika yanayofanya biashara na ulanguzi wa binadamu huko Laos, Kusini Mashariki mwa Bara la Asia.
Taarifa iliyotolewa na Serikali ya Burundi iliishukuru Serikali ya Kenya kwa kufanya operesheni kabambe iliyoratibiwa kwa pamoja na Serikali ya Laos na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM).
Kabla ya kufanyika kwa kazi hiyo, wiki mbili zilizopita Kenya ilifanikiwa kuwaokoa raia wake waliokuwa wakishikiliwa nchini Myanmar wakisubiri mpango wa kulanguliwa na kusafirishwa kuelekea katika maeneo mbalimbali duniani.
Hivi karibuni Ubalozi wa Burundi nchini Thailand, uliwatahadharisha raia wake kuwa waangalifu dhidi ya kazi za ualimu, biashara na huduma kwa wateja zinazotangazwa na kampuni za biashara zinazohitaji watu kutoka Afrika Mashariki.
Maofisa wa usalama wa Burundi waliwataka wananchi wote wa Burundi kujiridhisha na kuhakiki taarifa hizo ili kuthibitisha uhakika wa kile wanachoenda kufanya kabla ya kuondoka nchini.
Serikali za Kenya, Burundi na Uganda zimeeleza namna zinavyopokea simu mbalimbali kutoka kwa raia wake waliokwama katika nchi za Kusini Mashariki mwa Bara la Asia baada ya kuangukia kwenye mikono ya walanguzi.