Raia wa Marekani jela miaka 20 kwa ‘unga’

MAHAKAMA  Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imemuhukumu  Lione Lionel Rayford raia wa Marekani kifungo cha miaka 20 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin kiasi cha kilo 2.188.

Taarifa iliyotolewa leo Mei 27, 2023  na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na  Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imesema kuwa hukumu hiyo imetoka kufuatia shauri la uhujumu uchumi namba 17 la mwaka 2021 lililokuwa mbele ya Jaji Godfrey Isaya

Rayford alikamatwa  na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini Julai 5,  2018 katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere  akiwa ameficha dawa hizo katika moja ya mabegi aliyokuwa nayo.

Upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Clara Charwe, Erick Shija na Moses Mafuru Mawakili wa Serikali na jumla ya Mashahidi 15 wa upande wa Jamhuri walitoa ushahidi wao katika kuthibitisha kosa la mtuhumiwa kusafirisha dawa hizo wakati kwa upande wa utetezi uliwakilishwa na wakili Omari Kilwanda ambapo ulileta shahidi mmoja na mshitakiwa alijitetea mwenyewe.

Wakili Moses Mafuru aliwasilisha hoja za upande wa mashtaka za kuomba adhabu kali dhidi ya MtuhumiwaAlisema kiasi cha dawa kilikuwa ni kikubwa hivyo kilikuwa kinakwenda kuharibu na kuathiri sehemu kubwa ya jamii.

“Madhara ya dawa za kulevya kama yalivyo elezwa katika taarifa ya Mkemia Mkuu wa serikali yanasababisha ulevi usioponyeka, yana sababisha kuharibikiwa na akili na ni dawa ambazo zipo kwenye kundi la sumu, hivyo athari zake ni mbaya na zenye madhara makubwa kwenye afya ya binadamu.

” Alisema Mafuru

Pia, alisema matumizi ya dawa hizo yanaongeza uhalifu kwa maana ya kuongeza vibaka, wezi na hata wauaji, yanaharibu akili ya vijana ambao ni nguvu kazi katika ukuaji wa uchumi, hivyo kwa maana nyingine yanaharibu uchumi na ukuaji wa uchumi katika jamii.

Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizotia saini mikataba ya kimataifa ya kuzuia na kupambana na madawa ya kulevya hivyo mtuhumiwa kusafirisha madawa hayo ndani ya nchi ya Tanzania inaharibu taswira ya nchi katika maswala ya ushirikiano wa nchi kimataifa na diplomasia.

Habari Zifananazo

Back to top button