Raia wa Uganda akutwa na mihuri ya TRA, kilimo

JESHI la Polisi mkoani Kagera, linamshikiria raia wa Uganda akidaiwa kumiliki, kutumia  mihuri mitatu ya serikali kinyume na sheria  za nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari  mjini Bukoba, Kamanda wa Polisi mkoani humo, William Mwampaghale alisema mtuhumiwa amekuwa akitumia mihuri hiyo kugonga kwenye nyaraka mbalimbali

“Alikuwa akigonga hizo nyaraka kuonesha kuwa zimeidhinishwa na na idara husika ya serikali kwa maana ziko tayari kutoka nje kupitia mpaka wa Tanzania na Uganda, eneo la Mtukula,” alisema na kuongeza kuwa wameamua kuficha jina la mtuhumiwa, kwa vile bado wanatafuta wahusika wengine.

Advertisement

Alisema polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, waliandaa mtego na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa Septemba mosi saa 11 jioni Kijiji cha Mutukula, Wilaya ya Misenyi na kwamba alikutwa na mihuri hiyo mitatu aliyokuwa anaitumia mipakani.

“Mihuri hiyo ni ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ofisi ya Kilimo, ofisi ya mionzi na katika mahojiano mtuhumiwa amekiri kutumia kugongea kwenye nyaraka bandia, ambazo huzitumia kuvusha magari mbalimbali kwenda nchini Uganda, ” alisema.

Alisema hadi anakamatwa alishafanikiwa kuvusha magari aina ya fuso tisa na semi trailer mbili.