Rais Kagame ahimiza uzalishaji wa chai bora

RAIS Paul Kagame amewataka wakulima wa Rwanda kujitahidi kuzalisha chai iliyo bora na itakayoweza kushindana katika soko la dunia ili kuzipatia soko bidhaa mbalimbali zinazotoka nchini.

Kiongozi huyo aliyasema hayo baada ya kufanya ziara katika mashamba makubwa ya chai pamoja na Kiwanda cha Chai cha Rugabano kilichopo katika Wilaya ya Karongi ikiwa ni siku ya pili katika ziara ya siku nne katika Majimbo ya Kusini na Mashariki.

Aidha, Rais Kagame alisema kiwanda hicho kinafanya kazi kubwa na nzuri na ni muhimu kwa wananchi wa Rwanda kwa kuwa kinatoa ajira ya watu wengi na kupata fedha kwa ajili ya kulisha familia zao na kuwawezesha wawekezaji kulipa kodi kutokana na faida wanayopata.

“Umuhimu wa Kiwanda cha chai unadhihirika kutokana na ubora wa chai yetu si tu katika kanda yetu bali duniani kwa ujumla. Hii ni fursa tunayoweza kuitumia kuhakikisha kuwa tunavuna zaidi katika soko la dunia,” aliongeza Rais Kagame.

Kilimo cha chai kilianzishwa nchini Rwanda miaka ya 1950, mpaka mwishoni mwa mwaka 2021 kulikuwa na hekta zaidi ya 26,000 za mashamba ya chai nchini Rwanda. Kwa mujibu wa Bodi ya Chai ya Rwanda, uzalishaji wa chai umekuwa ukiongezeka kila mwaka.

Mpaka kufika mwaka 1980, Rwanda ilikuwa ikizalisha kiasi cha tani 5,910 na mpaka mwaka 1990 kulizalishwa tani 12,855 na hadi kufika mwaka 2021 Rwanda ilizalisha tani 36,000 za chai kwa mwaka na kuingiza kiasi cha dola za Marekani milioni 103.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button