Rais Mstaafu Kikwete amlilia Membe

RAIS Mstaafu wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu zake za rambirambi kwa Mke wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Mama Dorcas Membe akielezea alivyopokea taarifa za kifo cha Membe kwa mshtuko na huzuni kubwa.

RAIS Kikwete amesema “Nimemfahamu Membe miaka mingi, tumetoka nae mbali na tumesaidiana kwa mengi, familia zetu, na mapito ya maisha yetu yamehusiana sana, Bernard Kamillius Membe alikuwa ni mtu wa msaada mkubwa kwangu katika maisha yangu ya kikazi na kisiasa.

Amesema alimuamini na   kumtumainia katika nafasi zote alizohudumu kwenye Baraza lake  la Mawaziri.
“Aliwahi kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Mambo ya Ndani, na Wizara ya Nishati na Madini, aliwahi pia kuwa Waziri wangu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa miaka tisa,  alifanya kazi kubwa na zuri ya kuendeleza maslahi ya Tanzania katika medani za Kimataifa.
Advertisement

” Amesema na kuongeza

“Nautambua mchango wake mkubwa alioutoa kwenye Chama Cha Mapinduzi alipokuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Mjumbe wa Kamati Kuu na Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa katika Sekretariati ya Halmashauri Kuu ya Taifa, katika nafasi zote hizo, alijitoa kwa moyo wake wote na kuacha alama za Kudumu.

“Nilimfahamu Mheshimiwa Membe kama Mwanadiplomasia Mbobezi, Mwanamikakati makini, Msomi mzuri, Mcha Mungu, Mzalendo,Mchapakazi hodari na Mtu jasiri ambaye hakuogopa kusema na kulisimamia analoliamini.

“Hakika Taifa limepoteza mmoja wa watu wake muhimu, natoa salaam za rambirambi na mkono wa pole kwako Shemeji yangu Dorcas Membe na Watoto wenu Cecilia, Richard na Dennis, pamoja na Wajukuu, ndugu na jamaa wa marehemu Bernard Kamilius Membe, nawapeni pole kwa msiba mkubwa uliowakuta.

“Lakini napenda kuwahakikishia kuwa hamko wapweke, mimi pamoja na mke wangu Salma na wana familia wetu wote, tuko pamoja nanyi katika majonzi na kuomboleza, tunawaombea kwa Mola awajalie moyo wa subira na ustahamilivu katika kipindi hiki kigumu mnachopitia, tukumbuke daima.

“Sisi sote ni Waja wake, na kwake tutarejea” Bwana ametoa, Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe, Tumuombee kwa mola marehemu mpendwa wetu, apumzike kwa amani na Roho yake aiweke Mahala Pema Peponi. Amina”
Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *