Rais Mwinyi aitaka Tantrade kufanya tafiti

RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi ameitaka Mamlaka ya Biashara Tanzania (TanTrade) kufanya utafiti wa  uhakika kubaini masoko mapya ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi, na kutoa taarifa hizo kwa Wafanyabiashara ili waweze kuyafikia masoko hayo kwa urahisi.

Aidha, ameagiza taasisi zinazosimamia biashara nchini katika serikali zote mbili kuondoa  urasimu na katika hilo serikali hizo zitashirikiana kukuza biashara na uwekezaji kwa kufanyia kazi maoni ya wafanyabiashara nchini.

Rais Mwinyi, ametoa kauli hiyo leo Julai 13, 2023 akifunga Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam ‘Sabasaba 2023’ yaliyoanza Juni 28 mwaka huu.

Rais Mwinyi, amesema  “Maonesho ya mwaka huu yameenda na dhamira za serikali zetu, kufungua nchi katika masoko mbalimbali na kufungua nchi na fursa za uwekezaji.”Amesema na kuongeza

“Wigo wa masoko umepanuka na kutoa fursa ya kufanya biashara na nchi za jumuiya nane za Afrika,Tantrade fanyeni tafiti za uhakika wa masoko mapya ya bidhaa na leteni taarifa kwa wafanyabiashara wazichangamkie,”amesema.

Pia, amewataka watanzania  kutumia fursa ya masoko ya Jumuiya ya Afrika likiwemo soko la Eneo Huru la Soko Afrika (AfCFTA),SADC na la Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya biashara ya bidhaa zinazozalishwa nchini.

Katika hatua nyingine, Rais Mwinyi, amewataka |watanzania kuwa tayari kujifunza teknolojia mpya watakazozitumia kukuza biashara zao.


“Wakati huu tunapojiimarisha kiuchumi tuhakikishe tunajifunza teknolojia mpya na kuongeza ukuaji wa biashara kwa bidhaa mbalimbali kwa kutumia malighafi na rasilimali za ndani ya nchi kama vile mazao ya kilimo, uvuvi, misitu, madini, nishati ya gesi na makaa ya mawe”. Amesema Rais Dkt. Mwinyi

Pia ameushukuru uongozi wa Mamlaka ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa kuipa Zanzibar siku maalum katika maonesho hayo na kusema kuwa ana imani Wafanyabiashara wamepata fursa ya kujifunza kwa wageni.

“Ni matumaini yangu kuwa washiriki mmetumia vizuri fursa ya maenesho ya mwaka huu katika kukuza mahusiano ya kibiashara kati yenu pamoja na wageni walioshiriki maonesho”. Amesisitiza Dkt. Mwinyi.

Aidha, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Zanzibar, Omar Said Shaaban amesema, Zanzibar inaendelea na mipango yake ya kuandaa maonesho ya kudumu ya biashara katika eneo la Vumba  ambayo yatakuwa yakifanana na maonesho ya Sabasaba.

Habari Zifananazo

Back to top button