Rais Mwinyi awaita wawekezaji wa Ufaransa

ZANZIBAR: RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi ametoa wito na kuwakaribisha wafanyabiashara kutoka Ufaransa kuangalia fursa kuwekeza Zanzibar katika maeneo mbalimbali.

Dk Mwinyi amesema hayo leo Mei 29,2024 katika Ukumbi wa Hoteli ya Park Hyatty Zanzibar alipofungua mkutano wa majadiliano ya fursa za uwekezaji kati ya Ufaransa na Zanzibar kutoka kwa ujumbe wa Wafanyabiashara wa makampuni 20 ya Ufaransa.

SOMA: Kampuni 27 Ufaransa kuwekeza Tanzania

Rais Mwinyi amesema sera kuu ya uchumi wa Zanzibar ni uchumi wa buluu hivyo amewakaribisha kuangalia fursa za kuwekeza katika sekta ya utalii wa fukwe, urithi, michezo na mikutano, sekta ya bandari, mafuta na gesi, sekta ya bandari ikiwemo ya makontena , uvuvi pamoja na meli za usafirishaji wa mizigo na abiria.

Pia amebainisha fursa za miradi ya miundombinu ikiwemo barabara, viwanja vya ndege , sekta ya nishati na maji, pamoja na kilimo cha viungo.

Pia, Dk Mwinyi amewahikikishia wawekezaji hao kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mazingira mazuri kikamilifu ya kufanya biashara na uwekezaji.

Ujumbe huo pia uliambatana na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Nabil Hajlaoui , Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa Ali Mwadini na Mwenyekiti wa Shirika la Kimataifa la MEDEF kutoka Ufaransa, Gerald Wolf.

Viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Mawaziri na sekta binafsi wameshiriki mkutano huo.

Hivi karibuni, ujumbe wa wafanyabiashara kutoka kampuni 27 za Ufaransa upo nchini kwaajili ya kujadili fursa mbalimbali za uwekezaji.

Wafanyabiashara hao wanajadili namna ya kuwekeza Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwemo, teknolojia za miundombinu, nishati, usafirishaji na Maendeleo ya miji.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe akiwa jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano huo amesema mkutano huo ni muendelezo wa majadiliano yaliyofanywa na wafanyabiashara hao na Rais Samia Suluhu Hassan alipotembelea nchini huko Mei 2024.

Aidha ujumbe huo pia umesaini mikataba wa utunzaji wa mazingira pamoja na bayoanuai za misitu baina yao na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

SOMA: Kigahe: njooni muwekeze fursa zipo

Amesema ziko fursa kubwa za masoko nchini Ufaransa kwa bidhaa za kahawa,samaki za aina mbalimbali na hata mbegu za mbogamboga na kuwataka wananchi kuchangamkia eneo hilo.

Kigahe amesema serikali iko tayari kukaribisha wawekezaji kutoka Ufaransa  jambo litakalokuza uchumi wa Tanzania .

“Licha ya uwekezaji huo nchini lakini kuna fursa za masoko kwa bidhaa za Tanzania jambo linaloongeza wigo wa kuuza kwa wingi nchini humo,” amesema.

Amesema Kwa mujibu wa takwimu za Kituo Cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Ufaransa imewekeza Tanzania katika miradi 41 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 104.34 ambayo imetoa ajira 2379.

Amesema kampuni za Ufaransa zilizowekeza Tanzania ni katika maneno ya kilimo, ujenzi, usafirishaji, huduma,taasisi ,a fedha pamoja na rasilimali watu.

 

Habari Zifananazo

Back to top button