DAR ES SALAAM: Rais Samia Suluhu Hassan ameipongeza Kampuni ya Magazeti ya Serikali Tanzania (TSN) akisisitiza kuwa anaridhika na kazi zinazotekelezwa na kampuni hiyo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema.
Akizungumza muda mfupi baada ya kukagua ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha uchapaji kilichopo eneo la Sandali, Barabara ya Nelson Mandela jijini Dar es Salaam, Nape amesema Rais Samia ambaye ndiye Mhariri Mkuu wa Magazeti ya Daily News, HabariLEO na SpotiLeo “anafurahishwa” na mwenendo wa utendaji kazi wa chombo.
Waziri Nape amesema nia ya serikali ni kuona TSN inakuwa zaidi ya Chombo cha Habari na ndio maana imewekeza katika ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kisasa cha uchapishaji kibiashara.