‘Rais Samia ameipaisha sekta ya uwekezaji’

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni malkia wa nguvu na kwamba ameiwezesha sekta ya uwekezaji kung’ara na kwamba uchaguzi wa mwakani uwe wa wabunge na madiwani tu.

Kitila ameyasema hayo usiku wa kuamkia leo katika Tuzo za Malkia wa Nguvu zilizofanyika ukumbi wa Mlimani
City jijini Dar es Salaam.

“Rais Samia ni Malkia wa nguvu ameifanya sekta ya uwekezaji imeng’ara, uchaguzi wa mwakani ni wa madiwani na wabunge, Rais tayari tunae, ” amesisitiza.

Amesema, chini ya uongozi wa Rais Samia serikali imeweza kufanya maboresho 605 ya kisera, kisheria, kikanuni ili kuvutia wawekezaji.

Amesema, maboresho 416 sawa na asimilia 64 yalilenga kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji nchini huku maboresha 460 kati ya maboresha 665 yamefanyika kati ya mwaka 2022- 2023 sawa na asilimia asilimia 70.

Prof Kitila amesema maboresho hayo yamefanyika ili kuvutia wawekezaji ambao wamekuwa wakiangalia utulivu wa kisiasa na amani katika nchi husika, mazingira ya kisheria hususani kwenye ulinzi wa mali mwekezaji atawekeza kwenye nchi husika.

Naye, mwanasiasa nguli nchini Getrude Mongela akizungumza mara baada ya kupata Tuzo ya Heshima aliwataka mawaziri vijana kumsaidia Rais Samia kazi, ili kufikia lengo la kuhakikisha uchumi wa Tanzania unapaa na maisha bora kwa Watanzania.

Akiwashika mikono Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye na Prof Kitila Mkumbo, Mongela amesema “Nyie vijana endeleeni kushikana mikono, kuinuana, mawaziri mfuate nyayo zetu, Samia akianguka mimi na nyie, nchi inatekeleza yale tuliyotamani, muacheni mama Samia afanye kazi, maneno maneno muache, sisi tunataka amani, ” amesema na kuongeza

” Kama mnataka urais subirini miaka ijayo, lakini mwakani ni Rais Samia, ” amesisitiza.

Katika tuzo hizo, Profesa Esther Mwaikambo alipata tuzo Sekta ya Afya, Tuzo ya Uongozi katika Sekta ya Utumishi wa Umma mshindi ni Dk Lucy Shule ambae ni Mkurugenzi wa Mafunzo katika Chuo cha Ulinzi cha Taifa (NDC).

Pia tuzo ya uongozi ya Sekta Binafsi mshindi ni Rosemary Kacungira ambae ni mmiliki wa kampuni ya Equity Aviation na chuo cha marubani cha Soma Aviation huku tuzo ya Uongozi wa Huduma za Jamii mshindi ni Brenda Msangi Mkurugenzi Mtendaji wa CCBRT.

Tuzo ya Uvumbuzi na Ubunifu imeenda kwa Wilhelmina Kubingwa, Mkurugenzi wa Primina Investments wakati tuzo ya Funguo ya Maisha imeenda kwa mwanahabari mkongwe, Eda Sanga.

Habari Zifananazo

Back to top button