MOROGORO: KAMATI ya Kudumu ya Bunge , Ardhi , Maliasili na Utalii imeridhishwa na utekelezaji wa kazi za miradi ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Covid -19 iliotekelezwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania ( TAWA).
Mamlaka hiyo kupitia mpango huo iliidhinishiwa Sh bilioni 12.9 kati ya fedha hizo Sh bilioni 9.2 ni kwa ujenzi wa miundombinu kwenye miradi 32 , Sh bilioni 3.7 ununuzi wa magari sita , mitambo mitatu na boti za kisasa sita.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Timotheo Mnzava alitoa pongezi kwa Mamlaka hiyo baada ya kutembelea na kufanya ukaguzi wa miradi uliyokamilika eneo la Pori la Akiba Wami- Mbiki ambalo kwenye Mkoa wa Pwani kwa asilimia kubwa pamoja na Morogoro.
Hivyo alimpongeza Rais , Dk Samia Suluhu Hassan kwa ubunifu wake wa kutafuta fedha na maelekezo aliyoyatoa juu ya matumizi ya fedha hizo za Covid -19 ambazo zimeleta mapinduzi makubwa katika sekta utalii na nyinginezo .
“ Tunampongeza kwa ubunifu mkubwa alionao kwa kutafuta fedha kwa sababu miradi mingi imetekelezwa kwa kutumia fedha Covid-19 na ndiye aliyezitafuta na kuzitolea maelekezo namna gani zitumike” alisema Mnzava.
“ Kwa mazingira na hali tuliyoiona kwenye Pori hili la Wami – Mbiki nadhani tutaungana sote kumpongeza kwa dhati Rais wetu Dk Samia kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye nchi yetu” alisisitiza Mnzava .
Mwenyekiti wa kamati huyo alitoa wito na ushauri kwa wizara kuongeza mikakati ya kibiashara na ya kimasoko kutangaza mapori hayo ili miundombinu iliyotengenezwa itumike ilivyokusudiwa kwa ajili ya kupata tija iliyotarajiwa.
Naye Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula alisema wizara imejipanga kuhakikisha inaongeza jitihada katika kutangaza hifadhi hiyo ili kuongeza idadi ya wageni ikiwa ni pamoja na kutafuta wabia wa kushirikiana nao katika kuendesha shughuli za utalii na uwekezaji.
Kitandula alisema Mamlaka hiyo ilikabidhiwa pori hilo kwa ajili ya kuliboresha , kulirejesha katika hali yake ya uoto wa asili na kuhakikisha idadi ya wanyamapori kwa kwenye pori hilo inaongezeka.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka hiyo , Mabula Misungwi Nyanda aliithibitishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi , Maliasili na Utalii , kuwa miradi yote iliyokuwa inatekelezwa kwa kiasi hicho cha fedha imekamilika.
TAWA iliidhinishiwa kiasi cha Sh bilioni 12.9 na kati ya fedha hizo Sh bilioni 9.2 ni kwa ujenzi wa miundombinu kwenye miradi 32 , wakati Sh bilioni 3.7 ni ununuzi wa magari sita , mitambo mitatu na boti za kisasa sita.
Nyanda alisema ,kwa hivi sasa wameendelea kuzishikilia fedha za Covid-19 Sh milioni 19.8 ambazo ni za matazamio ya mradi (Retention) ya ujenzi wa daraja la Pori la Akiba Mpanga Kipengere ambalo kipindi cha matazamio ( Defects Liability Period ) kitakamilika Agosti 2024.
“ Ninakuhakikishia Mwenyekiti wa Kamati sisi miradi yote iliyokuwa inatekelezwa chini ya fedha za Covid-19 tumeikamilisha “ alisema Kamishna Nyanda.