Rais Samia amfuta kazi bosi ndege za serikali

Ataka hatua ripoti za CAG

RAIS Samia Suluhu Hassan amemfuta kazi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), Mhandisi John Nzulule siku chache tangu aonekane kukerwa na maombi ya malipo ya mwisho ya ndege ya mizigo kutoka dola za Marekani milioni 37, hadi milioni 86.

Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Rais Samia amemfuta kazi Nzulule na pia ametengua Bodi ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) baada ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kubaini dosari katika shirika hilo.

Kwa mujibu wa ripoti za ukaguzi za CAG, Charles Kichere, Shirika hilo lilimkataa Mzabuni aliyetaka kulipwa Sh bilioni 616.4 na kumpa kazi Mzabuni wa Sh trilioni 1.119 sawa na ongezeko la Sh bilioni 503.2 (asilimia 82) isiyokuwa na ulazima

Pia, katika ununuzi wa ‘Locomotives’ na Makochi ya Abiria, Shirika la Reli (TRC) lilitekeleza Mkataba bila dhamana ya Utendaji na kusababisha hasara ya Sh bilioni 13.7 kutokana na Mkandarasi kushindwa kutimiza Masharti ya Mkataba

Rais Samia amemtaka Katibu Mkuu Kiongozi kuhakikisha Makatibu Wakuu na Watendaji Wakuu wa taasisi wanaipitia kwa kina taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kujibu na kuzifanyia kazi kwa haraka hoja zote zilizogusa maeneo yao.

Ametaka watendaji wote watakao bainika kuhusika na uzembe na ubadhirifu kuchukuliwa hatua.

Habari Zifananazo

Back to top button