Rais Samia amlilia Jecha, Dk Mwinyi aongoza maziko
RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameongoza mamia ya waombolezaji wakiwamo viongozi wa serikali na vyama vya siasa kumzika aliyekuwa Mwenyekiti mstaafu wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha. Jecha aliaga dunia jana katika Hospitali ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo, Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Alizikwa kijijini kwao Kibeni Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja. Jecha alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuanzia mwaka 2013. Rais wa Zanzibar, Dk Mwinyi alitoa pole kwa familia na kuisihi iwe na subra na uvumilivu katika kipindi kigumu cha msiba. “Ni msiba mkubwa… natoa pole kwa ndugu wa familia na kuwataka kuwa na subra katika kipindi kigumu cha msiba,” alisema.
Pia Rais Samia Suluhu Hassan alituma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki kutokana na kifo hicho. Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari, Rais Samia alipokea taarifa za kifo cha Jecha kwa majonzi na masikitiko makubwa. Vilevile alituma salamu za rambirambi kwa familia ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, hayati Benjamin Mkapa baada ya kifo cha Bernard Mkapa (Mwenye Mkuti) ambaye alikuwa kaka yake.
Rais Samia aliwaomba wanafamilia wote wawe na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi. Mwenyekiti wa chama cha Ada Tadea Taifa, Juma Ali Khatib alisema Jecha atakumbukwa katika utendaji wa utumishi wake katika kuisimamia ZEC.
Kwa mfano alisema Jecha atakumbukwa kwa kufuta Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 na kutoa sababu kwamba taratibu nyingi za uchaguzi zilikiukwa wakiwamo mawakala wa vyama vya siasa kutokuwapo katika vituo kwa mbinu mbalimbali.
“Namkumbuka Jecha alinikabidhi fomu ya Urais wa Zanzibar katika uchaguzi wa mwaka 2015…lakini yeye ndiye aliyefuta uchaguzi wa mwaka huo kwa madai ya kuwapo kwa dosari nyingi za ukiukwaji wa sheria za uchaguzi,” alisema. Aidha, aliyekuwa Mwenyekiti wa chama cha ADC, Hamad Rashid Mohamed alimtaja Jecha kuwa ni kiongozi anayesimamia sheria na hakusita kubadilisha maamuzi makubwa kwa kuzingatia taratibu.
“Kiongozi anayekabidhiwa taasisi, tunapaswa kuheshimu maamuzi yake anayotoa japo wengine hawatakubaliana nayo lakini ndiyo maamuzi,” alisema Mohammed. Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar katika kipindi ambapo uchaguzi ulifutwa, Vuai Ali Vuai alisema Jecha alikuwa kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele katika uwajibikaji wa kuzingatia sheria na misingi yake. Historia Jecha alizaliwa mwaka 1952 kijijini kwao Kibeni Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja na kupata elimu ya msingi na sekondari kijijini kwao Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alipata elimu ya juu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika mwaka 1977 kwa kupata shahada ya kwanza. Shahada ya pili aliipata nchini Marekani na aliporudi nchini alianza kazi ya kufundisha. Baadhi ya nyadhifa alizoshika katika utumishi wa serikali ni Naibu Katibu Mkuu Wizara Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika miaka ya 1997.
Mwaka 2013 aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alimteua kuwa mwenyekiti wa ZEC.