RAIS Samia Suluhu Hassan amempongeza Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora, Protase Rugambwa kwa kuteuliwa kuwa Kardinali. Katika ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa twitter Rais Samia aliandika: “Nakupongeza Askofu Mkuu Protase Rugambwa kwa kuteuliwa na Baba Mtakatifu Fransisko kuwa Kardinali.
Naungana na Watanzania wote kukutakia kheri na kukusindikiza katika sala, unapoendelea na kazi yako ya utume katika hatua hii mpya”. Aliongeza: “Mwenyezi Mungu ambaye amekuinua kwa baraka na jukumu hili kwenye wito wako, aendelee kukuongoza katika kulitumikia Kanisa na jamii yetu kwa ujumla”.
Jana saa saba mchana Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis alimteua Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, Mhashamu Protase Rugambwa kuwa Kardinali. Kuteuliwa kwa Askofu Mkuu Mwandamizi Rugambwa, kunalifanya Kanisa Katoliki nchini Tanzania kufikisha maaskofu watatu walioteuliwa kuwa makardinali.
Wa Kwanza ni aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar er Salaam, Laurean Rugambwa, Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na sasa Askofu Mkuu Mwandamizi Rugambwa.
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk Charles Kitima na Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Method Kilaini walisema kwa nyakati tofauti kuwa, Tanzania sasa itakuwa na makardinali wawili walio hai na wote wakiwa na sifa za kupiga kura kuchaguliwa au kuchagua Papa mpya.
“Kwa sasa Mwadhama Pengo amestaafu mamlaka kama Askofu Mkuu wa Jimbo la Dar es Salaam, lakini bado ni kardinali anayefanya kazi na anaweza kuchaguliwa au kuchagua papa maana hajafikisha miaka 81,” alisema Padri Kitima.
Akaongeza: “Baba Mtakatifu ameona Kanisa la Tanzania lina mtu mwingine anayeweza kumshauri na kumsaidia katika kulihudumia Kanisa la kidunia. Tumshukuru Mungu na kumtakia kardinali mpya majukumu mema ili atimize imani ya Papa kwa kuitendea haki kupitia utume wake.”
Askofu Kilaini alisema bila shaka Rugambwa amefanya kazi nzuri akiwa Vatican ndio maana kanisa limempa wadhifa huo. Aidha, Kilaini alifafanua uhusiano wa jina la hayati Rugambwa na Kardinali Mteule Rugambwa akisema viongozi hao wa kanisa si ndugu.
“Jina lao halitokani kwamba ni ndugu; hapana. Hawa si ndugu, bali linatokana na kumbukumbu kwani siku hayati Kardinali Rugambwa anawasili jimboni Bukoba kutoka Vatican kupewa majukumu na kofia ya ukardinali kukiwa na mapokezi jimboni, ndio siku hiyo aliyozaliwa kardinali huyu mpya Rugambwa hivyo wazazi wake waliokuwa Wakatoliki, wakampa jina la Rugambwa kama kumbukumbu ya mapokezi ya siku hiyo,” alisema.
Dk Kitima alisema kanisa litapanga siku na namna ya kumpokea, lakini akadokeza akisema Septemba 30, mwaka huu Papa Francis atampa majukumu rasmi ya ukardinali huko Vatican. Akaongeza: “Tofauti na teuzi nyingine za maaskofu ambazo Papa huagiza nchi kupitia Baraza la Maaskofu kumtangaza askofu mteule, uteuzi wa kardinali hufanywa na Baba Mtakatifu mwenyewe kama alivyofanya leo (jana) saa saba wakati wa Sala ya Mchana.”
Askofu Kilaini na Padri Kitima walisema hakuna idadi maalumu makardinali kwa nchi moja kwa kuwa inaweza kuwa na kardinali mmoja, isiwe naye kabisa au ikawa na makardinali zaidi ya mmoja. Kuhusu nafasi yake ya Askofu Mkuu Mwandamizi wa Tabora, Askofu Kilaini alisema kwa sasa ataendelea kuwa askofu mwandamizi na hata ikitokea baadaye akawa Askofu Mkuu mwenye Jimbo si lazima aje Dar es Salaam.
Askofu Mkuu Protas Rugambwa alizaliwa Mei 31, 1960 katika Kijiji cha Bunena mkoani Kagera. Alipata upadri Septemba 2, 1990 na kuwa Padri wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara. Aprili 13, mwaka huu, Papa Francis alimteua kuwa Askofu Mkuu Mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo Kuu Katoliki la Tabora. Juni 25 mwaka huu baada ya waumini kumpokea katika Jimbo Kuu Katoliki Tabora Askofu Mkuu Mwandamizi Rugambwa alimshukuru Mungu kwa neema ya wito wa kumtumikia akiwa Padre na Askofu katika sehemu mbalimbali.
“Nimejikuta naitwa na Mwenyezi Mungu nimtumikie hapa na pale nami nikiamini katika majaliwa na maombezi yake nimejitahidi kuitikia mara zote hata kama wakati mwingine nimejitkuta nikihoji na kusita na kuogopa,” alisema.
Aliongeza: “Fursa hii naiona kama mwanzo wa awamu mpya katika maisha yangu ya wito na utumishi huku nikiyakumbuka kwa moyo wa shukurani, ninayapokea sasa kwa moyo radhi na kwa hamasa nikitazamia ya mbeleni kwa imani kubwa na matumaini kwani Yesu Kristu aliyeniwezesha kutekeleza yaliyopita ni yuleyule jana, leo na milele”.
Kabla ya kuteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Tabora, kwa miaka 10 Askofu Mkuu Rugambwa alikuwa kiongozi katika idara ya uinjilishaji kwenye Makao Makuu ya Kanisa Katoliki Vatican nchini Italia.
Kabla ya hapo alikuwa mtumishi wa kawaida Vatican kwa miaka sita.
Pia katika uteuzi huo, Papa Francis amemteua aliyewahi kuwa Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Tanzania, Agustino Machetto kuwa Kadinali.
Wakizungumzia uteuzi huo, Herman Lwagila wa Ubungo- Dar es Salaam, Zainabu Mbinga wa Parokia ya Ukonga na Christopher Dikola wa Parokia ya Mwenge katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam walisema uteuzi huo ni heshima kwa Watanzania
Comments are closed.