Rais Samia apewe maua yake

JAMHURI ya Muungano wa Tanzania-Kazi Iendelee.

Mei Mosi kulifanyika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi duniani, kama ilivyo kawaida ya siku zote inapofika tarehe na mwezi huo.

Kitaifa siku hiyo iliadhimishwa mkoani Morogoro ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika sherehe hizo kwa mara nyingine tena Rais Samia aliendelea kuonesha uthabiti wa kauli zake na kutimiza mambo ya wafanyakazi wa Tanzania kama ambavyo amekuwa akiwaahidi.

Je, unayafahamu mambo 6 muhimu yaliyojiri siku hiyo? Fuatilia:

  1. Arejesha nyongeza ya mishahara kila mwaka

Miongoni mwa jambo kubwa kabisa lililotamalaki na kutamakani katika vyumba vya habari ni hili la kurejesha nyongeza ya mishahara kila mwaka ambayo ilisitishwa.

Rais alisema: “Niseme pia kuna nyongeza za mishahara za mwaka ambazo kwa muda mrefu zilikuwa zimesitishwa nikaona mwaka huu tuzirudishe, kwa hiyo wafanyakazi wote mwaka huu mbali na niliyoyasema kupanda madaraja na mambo mengine lakini kuna nyongeza ya mishahara ya kila mwaka, na tutaanza mwaka huu na tutakwenda kila mwaka kama ilivyokuwa zamani.”

Hatua hii imeelezwa kuwa ni muhimu sana kwa wafanyakazi ambapo utaratibu wa nyongeza yao ya kawaida kwa kila mwaka (annual increments) itarejeshwa.

  1. Posho ya ufundishaji kwa walimu

Rais Samia pia ameonesha nia na ari kubwa kusaidia suala la posho hiyo kwa walimu. “Suala la ‘teaching allowance’ (posho ya ufundishaji) tumelichukua, unajua walimu ni jeshi kubwa katika nchi hii…tumelichukua, tutakwenda kuliangalia uwezo wa nchi halafu tuone tunafanyaje,” alisema rais kwenye sherehe hizo.

Kwa hakika hii ni hatua kubwa kwa Rais kulipokea suala la walimu.  Kwa tajriba ya kichambuzi niseme tu kwa namna Rais alivyo mthabiti wa kauli ni dhahiri siku si nyingi jambo hili nalo atalifanyia kazi ipasavyo.

  1. Nyongeza ya mishahara asilimia 23, posho

Rais Samia pia amefafanua nyongeza hiyo ambayo aliitoa kwa wafanyakazi kuwa iliwagusa watumishi kwa viwango tofauti tofauti.

Katika hatua nyingine alidadavua kuwa nyongeza ya posho ilipotolewa bajeti ilikuwa imekwishapita lakini kwa bajeti ya sasa mambo yatakuwa bulbul.

  1. Nyongeza za mishahara kuendelea

Rais Samia amesema pia atazidi kushughulikia zaidi shida za wafanyakazi ikiwamo kuongeza mishahara. Ila hilo litafanyika kimya kimya ili kulinda mfumuko wa bei hasa pale wafanyabiashara wanaposikia kuwa mishahara imeongezeka.

Suala hili ni muhimu sana. Aghalabu imekuwa jambo la ada kwa wafanyabiashara, wamiliki wa nyumba na wadau wengine wasikiapo kuna ongezeko la mishahara wamekuwa wakiongeza bei za mapango na bidhaa mbalimbali kihobela hobela.

Tiba hii ya Rais Samia huenda ikapunguza au kuondoa kabisa suala hili.

  1. Shukrani kwa wafanyakazi kukuza uchumi

Rais Samia ameonesha kongole kwa wafanyakazi wote kwa juhudi yao katika kupiga kazi kubwa kwa bidii.

Ripoti ya hivi karibuni ya Benki ya Dunia na hata Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limeonesha uchumi wa Tanzania umezidi kuimarika.

“Ripoti kutoka Benki ya Dunia inasema Tanzania uchumi wake unazidi kuimarika kadri siku zinavyozidi kwenda, hizi ni juhudi kutoka kwa wafanyakazi wote nchini,” anasema Rais Samia.

Huu ni uungwana wa hali ya juu na ni kuonesha ni kwa namna gani Rais Samia anaendesha serikali shirikishi na kutoa shukrani kwa wafanyakazi.

  1. Kaulimbiu ya maadhimisho

Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ilikuwa ni ‘Mishahara Bora na Ajira za Staha na Nguzo kwa Maendeleo ya Wafanyakazi, Wakati ni sasa’.

Kwa hakika ukiichunguza kwa jicho pevu kaulimbiu hii unaona imeletwa wakati mwafaka.

Kwani Rais Samia kwa hakika amekuwa mstari wa mbele katika kushughulikia mishahara bora, ajira za staha na maslahi ya wafanyakazi kama tulivyobainisha hapa chinini.

Katika hatua nyingine pamoja na mambo mengine kama ilivyo ada sherehe hizo zilihanikizwa na mabango mbalimbali ya wafanyakazi na mifano ya shughuli za kazi mbalimbali wazifanyazo.

Jambo la pekee ni kuona baadhi ya mabango yalionesha namna Rais Samia na serikali yake waliyoyafanya katika utekelezaji wa shida anuwai za wananchi.

Mathalani, bango la wafanyakazi wa mamlaka ya maji liliandikwa:

‘Mama umeitendea haki sekta ya maji ndani ya miaka 2’

-Umenunua mitambo 25 ya kuchimba visima virefu

-Umenunua seti 5 ya kujenga mabwawa

-Umejenga na kukamilisha miradi 1,192

-Vijiji vipya 2,005 vinapata maji n.k.

Kwa hakika Rais Samia anaendelea kuinua wafanyakazi kwa kushughulikia changamoto zao mbalimbali ambapo hali hiyo imesaidia kuimarisha utendaji bora wa wafanyakazi na kuongeza ari na bidii ya kuchapa kazi.

Baadhi ya mambo aliyowahi kuyashughulikia ndani ya miaka 2 ni pamoja na yafuatayo kama ambavyo tumewahi kuyachambua katika makala zetu za huko nyuma.

Aliongeza mshahara kwa ongezeko la asilimia 23.3, alipunguza kodi ya mshahara (payee) kutoka asilimia 9 hadi 8, aliongeza ajira mpya zaidi ya 50,000.

Alipandisha madaraja kwa watumishi 190,562, alilipa malimbikizo ya mishahara, alilipa mafao ya wastaafu kwa wakati.

Alifuta tozo ya asilimia 6 ya Bodi ya mikopo ya elimu ya juu, aliongeza  umri wa utegemezi wa mtoto kutoka miaka 18 hadi 21 katika kugharamia matibabu yao, alifanya marekebisho ya Sheria ya Bodi ya walimu, alifanya ubadilishwaji wa kada na miundo ya utumishi. Ambapo watumishi zaidi ya 21,204 walinufaika na suala hilo, alipandisha vyeo watumishi 198, 215.

Hivi ndivyo ambavyo Rais Samia ametekeleza ahadi zake kwa vitendo na kuonesha uthabiti wa kauli zake. Kwa hakika mama ameleta faraja kwa watumishi na Watanzania kwa ujumla.

Ndio maana tunasema kwa lugha ya kileo ‘Mama apewe maua yake tu’ yaani, kongole zinazomstahiki.

Ni imani yetu kuwa kushughulikiwa kwa masuala haya ya wafanyakazi na Rais Samia yataongeza chachu na kuchochea bidii na juhudi kubwa ya kazi ili kuzidi kuimarisha zaidi uchumi na suala la maboresho zaidi kwa wafanyakazi liendelee.

Pia, itaamsha bidii na juhudi zaidi kwa wafanyakazi katika kuwahudumia wananchi ipasavyo.

Vilevile iwe chachu ya kuongeza ubunifu na ugunduzi wenye tija kwa maisha ya Watanzania wote.

Kongole sana Rais wetu, twakuombea siha Mola akutunze. Amina.

Mwandishi ni Mhadhiri na Mshititi kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere- Kampasi ya Kivukoni.

sovu82@gmail.com

0713400079

Habari Zifananazo

Back to top button