Rais Samia asamehe wafungwa 376

RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa msamaha kwa wafungwa 376 wanaotumikia vifungo katika magereza kwa makosa mbalimbali ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iliyotolewa jana, wafungwa hao wamegawanyika katika makundi mawili ambapo wako walioachiwa huru na wale waliopunguziwa robo ya adhabu zao.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa wafungwa sita waliachiwa huru jana na wengine 370 wataendelea kubaki gerezani kumalizia vifungo vyao baada ya kupunguziwa robo ya adhabu kama ilivyoagizwa na mheshimiwa Rais.

Robo hiyo ya adhabu ni nje ya punguzo la theluthi moja la kawaida linalotolewa chini ya kifungu cha 46(1) cha Sheria ya Magereza sura ya 58.

Wafungwa watakaopata msamaha ni wale ambao tayari wametumikia robo ya adhabu zao gerezani na waliingia kabla ya Februari 26, 2023 pamoja na wafungwa wa kike walioingia gerezani wakiwa na watoto wanaonyonya na wasionyonya.

Msamaha huo hautawahusisha wafungwa waliohukumiwa kunyongwa wala waliotiwa hatiani na kuhukumiwa kwa makosa ya kujaribu kuua, kujiua au kuua watoto wachanga.

Pia wasiohusika ni wafungwa wanaotumikia vifungo vya nje chini ya sheria ya bodi ya Parole, wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kujamiiana, utekaji au wizi wa watoto, kupoka, kuwapa mimba wanafunzi au makosa yoyote yanayohusiana na ukatili dhidi ya watoto na kujihusisha kwa namna yoyote na biashara ya binadamu hawatahusika na msamaha huo.

Wengine ni wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa makosa ya kukutwa na viungo vya binadamu, unyang’anyi, unyang’anyi wa kutumia nguvu, wa kutumia silaha, kumiliki silaha, risasi mlipuko au kujaribu kutenda makosa ya aina hiyo nao hawatuguswa na msamaha huo.

Wafungwa wengine wasiohusika ni wanaotumikia vifungo kwa makosa ya ujangili au kupatikana na nyara za serikali, wizi na ubadhirifu wa fedha au mali za serikali, kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali au kujaribu kusaidia kutendeka kwa makosa hayo, wafungwa waliowahi kupata msamaha wa Rais na kutenda makosa tena pamoja na wafungwa wa madeni.

Habari Zifananazo

Back to top button