Rais Samia ashukuru Bunge kwa kumuamini
RAIS Samia Suluhu Hassan amelishukuru Bunge kwa imani liliyoonesha kwake na kwa serikali.
Ameahidi kushirikiana nalo kutekeleza yaliyoainishwa kwenye mipango ya serikali na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema hayo bungeni Dodoma jana wakati anatoa maelezo kuhusu shukrani za Rais Samia kwa Bunge kwa kupitisha Azimio la Kumpongeza.
“Mtakumbuka Aprili 4, mwaka huu katika mkutano unaoendelea wa 11, Bunge lilipitisha Azimio la Kumpongeza Rais Samia kwa kuimarisha demokrasia nchini na kukuza demokrasia ya uchumi,” alisema Dk Tulia na kuongeza:
“Kutokana na azimio hilo, napenda kuwajulisha kuwa Rais Samia analishukuru Bunge kwa pongezi hizo kwake na imani iliyooneshwa na Bunge pamoja na serikali anayoiongoza.”
Aidha, alisema katika shukrani hizo, Rais ameahidi kuwa serikali itaendelea kutekeleza mambo yaliyopo kwenye mipango ya maendeleo na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/25.
Pia, alisema Rais Samia anaomba ushirikiano wa Bunge ili serikali iweze kutekeleza yaliyoainishwa kwenye mipango ya Serikali na Ilani ya CCM.
Mwanzoni mwa mwezi uliopita, katika mkutano wa Bunge la 11 unaoendelea, Bunge hilo liliazimia kumpongeza Dk Samia kwa kuimarisha demokrasia na kukuza diplomasia ya uchumi.
Bunge hilo liliazimia kumuunga mkono Rais Samia katika majukumu yake ya urais wa Tanzania na kumwombea afya njema, baraka na ulinzi wa Mwenyezi Mungu.
Mbunge wa Biharamulo, Ezra Chiwelesa (CCM) ndiye aliyesoma Azimio hilo bungeni Dodoma na kueleza kuwa katika miaka miwili ya uongozi wa Rais huyo hali ya demokrasia na utawala bora imeimarika nchini.
Chiwelesa alitaja mambo yaliyochangia kuimarika kwa demokrasia kuwa ni pamoja na uamuzi wa kuruhusu shughuli za siasa hasa mikutano ya hadhara kufanyika nchini kote.
Pia, alisema serikali kutekeleza huduma za kijamii na kiuchumi hususani masuala yanayogusa maendeleo ya wananchi na kuanzisha vikao vya maridhiano vya kisiasa miongoni mwa vyama vya kisiasa ili kuhakikisha kuna uhusiano mwema miongoni mwa makundi yaliyokuwa yakihasimiana.
Alitaja mambo mengine kuwa ni kuanzisha mchakato wa kufanya marekebisho ya kimfumo na kisheria yanayoongoza shughuli za kisiasa na kudumisha misingi ya amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Katika eneo la demokrasia alisema serikali inayoongozwa na Rais Samia imekuza demokrasia ya uchumi na yeye amekuza chachu ya mafanikio hayo kwa kuwa mwanadiplomasia mahiri.
Alisema diplomasia ya uchumi imeongeza masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini katika masoko ya nje, kuimarisha uhusiano wa kimkakati na kampuni za kimataifa unaolenga kuwekeza katika sekta za uzalishaji ili kuchochea ukuaji wa uchumi.