Rais Samia atajwa mafanikio TANROADS

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi Rogatus Mativila amesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo katika mwaka huu wa fedha 2022/23.

Mhandisi Mativila ameyasema hayo leo jijini Dodoma katika mkutano wake na wanahabari uliojikita kuelezea mafanikio ya TANROADS ambayo imekuwa mstari wa mbele katika usimamizi wa miradi mbalimbali ya miundombinu ya ujenzi wa barabara, madaraja na viwanja vya ndege.

Mhandisi Mativila amesema tangu kuanzishwa kwake, TANROADS imeweza kusimamia ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara kuu na za Mikoa zenye urefu wa kilometa 36,362.

“TANROADS imekuwa na mipango mingi ili kuhakikisha nchi inakuwa na barabara nyingi za lami ikiwemo kushirikiana na sekta binafsi kwa ajili ya kujenga barabara kwa kiwango cha lami,”  ameeleza.

Aidha, alisema kumekuwa na mafanikio makubwa ya ujenzi wa madaraja  na viwanja vya ndege chini ya uongozi wa Rais Samia kwakuwa  amekuwa mstari wa mbele kwa kutoa fedha kwa wakati na maelekezo bora  yaliyokuwa na ufanisi kwao.

Amesema TANROADS ilianzishwa kwa Waraka wa Serikali uliotolewa katika gazeti la Serikali Na. 293 la tarehe 25 Agosti, 2000 kwa mujibu wa Sheria ya  Wakala wa Serikali Na. 30 ya Mwaka 1997.

Malengo ya kuanzishwa kwa Tanroads ni kuleta ufanisi zaidi katika majukumu yaliyokuwa chini ya Idara ya Barabara ndani ya Wizara ya Ujenzi.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button