Rais Samia ataka matokeo kilimo biashara

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema serikali itatimiza ahadi yake kuwezesha vijana kulima kibiashara kupitia programu ya mashamba makubwa na hataki kusikia mradi huo umeshindikana.

Pia amesema anataka matokeo ya mradi huo na akaonya fedha anazotoa kwenye kilimo zisichezewe hata shilingi moja.

Rais Samia ametoa kauli hizo Dodoma wakati wa uzinduzi wa mashamba makubwa ya pamoja na vitendea kazi vya shughuli za kilimo ikiwa ni pamoja na mitambo, magari na drones (ndege nyuki).

Hafla hiyo pia ilienda sambamba na Rais kushuhudia utiaji saini kwenye mikataba 33 ya upembuzi yakinifu, usanifu, ujenzi na ukarabati wa skimu za umwagiliaji kati ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na wakandarasi ambayo itagharimu takribani Sh bilioni 146, miradi ambayo inatarajia kuanza katika mwaka wa fedha 2023/2024.

Pia Rais Samia alikabidhi hundi ya Sh milioni 200 kwa vijana wanaofanya kazi za kilimo waliokidhi vigezo.

Alisema uamuzi wa serikali kufanya uwekezaji huo ni mwanzo wa kuanza safari ya kuhakikisha kilimo cha mazao kuchangia asilimia 10 kutoka asilimia 4 kwenye Pato la Taifa ifikapo mwaka 2030.

“Safari hii haiwahusu vijana watakao husika na block farms (mashamba makubwa) pekee bali hata vijana, wanawake ambao kwa sasa wako mashambani tayari. Tulipotangaza mpango huu tayari tuna vijana zaidi ya 20,000 ambao wameomba kuingizwa kwenye mpango huu na pia tuna idadi kubwa ya vijana walioko mashambani,” alisema Rais Samia na kuongeza:

“Niwaombe sana vijana wangu, watoto wangu ambao wameingia katika mpango huu nendeni mkafanye kazi, serikali imejipanga kwa hili, yale yote mnayoyahitaji tutawapatia na kuyafanyia kazi, watoto wangu na mlioko mashambani nendeni mkalime kibiashara.”

Alisema dhamira yake ni kuona mradi huo unakuwa na mafanikio na si vinginevyo.

“Mimi nataka niwathibitishie kuwa dhamira yangu ni kuwa jambo hili nataka litokee na tumeanza na kuongeza bajeti ya kilimo na tutakwenda na mwendo huo huo miaka mingine iliyobaki,” alisema Rais Samia.

Alisema serikali itaendelea kukuza eneo la maofisa ugani na kuwa tayari imeshatoa vitendea kazi na mitambo na kuajiri wataalamu wa kilimo takribani 300.

“Nitakapotoa fedha za wavujajasho wa Tanzania ziende kwenye matumizi ya kilimo na fedha hiyo ikachezewa sitavumilia, nataka kuona kila shilingi itakayowekwa kwenye udongo, kila shilingi itakayowekwa kwenye sekta ya kilimo iende ikazalishe mara mbili au mara tatu,” alisema Rais Samia.

Aliagiza viongozi wa wizara hiyo watekeleze majukumu yao wakitilia maanani kuwa wanatekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo mambo mengi serikali imeanza kuyafanyia kazi.

Rais Samia pia ameagiza wizara za kisekta ziunde kamati ya kisekta ya mawaziri ili kuhakikisha programu hiyo inatekelezwa kikamilifu.

“Mtashindwa kama hamna dhamira, mkiwa na dhamira sioni mtashindwa wapi. Na sitaki kusikia tumeshindwa, lazima twende tufanye kazi na lazima tufanikiwe,” alisema.

Pia katika kuimarisha huduma za ugani, Rais Samia alisema serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ajira mpya ya sekta ya kilimo ikiwa ni mbali na wataalamu 300 ambao tayari wameshaajiriwa.

 

Habari Zifananazo

Back to top button