RAIS Samia Suluhu Hassan amemtaka Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, SACP Mzee Ramadhani Nyamka kuhakikisha haki katika usimamizi wa wafungwa na kutimiza wajibu wa msingi wa magereza, ambao ni kurekebisha tabia.
Rais Samia amesema jeshi la magereza linakabiliwa na changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni utawala bora na kumtaka Kamishna Jenerali Nyamka kupeleka maofisa wa magereza shule kwa ajili ya mafunzo.
“Kuna changamoto ya utawala wa kusimamia haki na kushindwa kufanya kazi ya msingi, ambayo ni kurekebisha tabia,” amesema Rais Samia. “Sio kila wanaoletwa huko ni wahalifu walio kubuhu hao pia ni binadamu.”
Kwa mujibu wa Rais Samia watu walioko magerezani wanapaswa kupata hewa nzuri, chakula na mavazi.
Rais Samia amesema serikali imeongeza bajeti ya jeshi hilo na hivyo ametaka tatizo la usimamizi wa fedha za umma likomeshwe.