Rais Samia atoa magari 13 ya wagonjwa Ruvuma

RAIS wa Samia Suluhu Hassan ametoa magari 13 kwa ajili ya kubebea wagonjwa na kufanyia usimamizi shirikishi katika sekta ya afya Mkoa wa Ruvuma.

Hayo yamesema na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dk Louis Chomboko kwenye hafla ya kukabidhi magari sita mapya,iliyofanyika katika viwanja vya ukumbi wa Chandamali mjini Songea.

“Awamu ya kwanza tulipokea magari saba na leo katika awamu ya pili tumepokea magari sita ili kutimiza lengo la magari 13 kati ya hayo magari tisa ya kubebea wagonjwa na magari manne ya usimamizi’’,alisema Dk Chomboko.

Akizungumza baada ya kukabidhi magari hayo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ametoa rai kwa watumishi wakiwemo madereva kuyatunza magari hayo kwa kuwa serikali imetumia fedha nyingi kuyanunua.

“Haitakuwa na maana yeyote baada ya miezi michache magari yanaharibika,hata nia njema ya Mheshimiwa Rais ya kuwasaidia watanzania itakuwa haina maana,naagiza magari yatumike kwa malengo yaliyokusudiwa,yasiwe magari ya kubebea mbolea Kwenda shambani au kubebea nyasa’’,alisisitiza.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amezindua kampeni ya chanjo ya surua na rubella ambayo imeanza Februari 15 na inatarajia kukamilika Februari 18,2024 ambapo zaidi ya watoto 200,000 wenye umri wa kuanzia miezi tisa hadi miezi 59 wanatarajia kupata chanjo hiyo.

Ugonjwa wa surua rubella upo mkoani Ruvuma ambapo takwimu za mwaka 2023 zinaonesha kuwa sampuli 135 zilipelekwa maabara,ilibainika kuwa sampuli 22 zilithibika kuwa na virusi vya ugonjwa wa surua rubella.

Habari Zifananazo

Back to top button