Rais Samia atoa suluhu kwa waliokosa mkopo elimu ya juu
RAIS Samia Suluhu Hassan ameridhia wanafunzi 28,000 waliokidhi vigezo waliopaswa kusajiliwa vyuoni waende vyuoni kuendelea na usajili chini ya uratibu wa Wizara ya Elimu wakati taratibu muhimu zikikamilishwa.
Akitoa hoja ya kuahirisha Bunge leo Ijumaa, jijini Dodoma, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaeleza wabunge kuwa miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa kwa hisia na kupewa uzito mkubwa na wabunge wakati wa mkutano huu ni hoja ya ugharamiaji, upangaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu.
“Nyote mtakubaliana nami kwamba lengo la mjadala huo, lilikuwa ni kutafuta suluhu ya suala la wanafunzi takribani 28,000 wenye uhitaji wa kupata mikopo ya Elimu ya Juu kwa mwaka 2022/23 ambao walikuwa hawajapangiwa mikopo, kutokana na ukomo wa kibajeti.
“Mheshimiwa Spika, lengo la Mheshimiwa Rais ni kuwanufaisha wanafunzi wote wenye uhitaji, waliopata udahili na wenye vigezo vya kupata mikopo. Katika mapitio ya bajeti ya nusu mwaka baadaye mwaka huu tutaliomba Bunge lako tukufu liridhie matumizi ya fedha zitakazohitajika,” ameeleza.
Akizungumzia hatua hiyo, Waziri Mkuu amesema lengo la Rais ni kuwanufaisha wanafunzi wote wenye uhitaji, waliopata udahili na wenye vigezo vya kupata mikopo.
“Katika mapitio ya bajeti ya nusu mwaka baadaye mwaka huu tutaliomba Bunge lako tukufu liridhie matumizi ya fedha zitakazohitajika,” ameongeza.
Kwa upande mwingine, Majaliwa amelieleza Bunge kuwa Serikali imeyapokea kwa mazingatio makubwa, maoni ya Waheshimiwa Wabunge na Maazimio ya Bunge yaliyotokana na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali iliyowasilishwa Novemba 5, 2022 kuhusu kuifanyia ukaguzi wa kina Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu katika mchakato mzima wa ugharamiaji, upangaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini.
“Hivyo basi, mara baada ya Timu hiyo kukamilisha jukumu hilo, taarifa yake itakuwa sehemu ya nyaraka muhimu kwa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kutekeleza Maazimio ya Bunge kuhusu ukaguzi wa ufanisi katika ugharamiaji wa elimu ya juu nchini,” ameongeza.
Amewasihi wabunge kutochoka kuishauri Serikali juu ya namna bora zaidi ya kugharamia elimu ya juu nchini kwa lengo la kuufanya utaratibu huo kuwa endelevu, fanisi na yenye tija.