Rais Samia azindua jengo la Safina
Ataka kufundisha maadili kwa vijana
RAIS Samia Suluhu Hassan amezindua mesifu jengo la kitega uchumi la Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Central Tanganyika lililopewa jina la Safina House jijini Dodoma.
Jengo hilo ambalo tayari limeshapata wapangaji ikiwemo Benki ya NMB litakuwa likiingiza mapato ya shilingi bilioni moja kwa mwaka na limejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni nane.
Akizindua jengo hilo leo Agosti 15, 2023 mjini Dodoma, Rais Samia amesema jengo hilo limebadili mandhari na kuwa ya kupendeza.
“Jengo hili la kitega uchumi ni la aina yake kwa usanifu na mwonekano wake, nimefika hapa leo nikasema wao, nimejitahidi kufanya michoro mizuri kule Magufuli City, lakini hapa mmenipiga kidogo, kwa hiyo tutashirikiana na wachoraji waje watuchoree mengine ambayo yanaendelea kujengwa hapa Dodoma,”amesema Rais Samia
Aidha, amelitaka Kanisa hilo kuendelea kulinda maadili, kukemea maovu na kufundisha maadili kwa vijana pamoja na kukemea watu wazima wanaolitumia Kanisa kufanya mambo ya hovyo.