Rais Samia, Hichilema wawakumbuka mashujaa Zambia

ZAMBIA; Lusaka. RAIS Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, wameongoza mamia ya wananchi wa Zambia katika dua na kuweka mashada ya maua kwenye mnara wa mashujaa uliopo la mtaa wa Uhuru Lusaka, Zambia.

Pamoja na mnara huo wa mashujaa pia Rais Samia aliweka mashada ya maua katika kaburi la muasisi na baba wa Taifa hilo, Kenneth Kaunda.

Aidha, viongozi wa dini, mabalozi, ndugu wa mashujaa waliopoteza maisha na viongozi wa Kitaifa wa Taifa hilo waliweka mashada katika mnara huo.

Katika tukio hilo lililohudhuriwa na viongozi wa Kitaifa wa nchi hizo mbili na wananchi, jambo kubwa lililosisitiziwa ni kudumisha amani na ushirikino wa kidugu baina ya nchi hizo.

Shughuli hiyo iliongozwa na Jeshi la Zambia kwa maandamano ya gwaride na vikundi vya asili vya akinamama.

Awali, Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema alianza kuwasili eneo  Kamwala jijini Lusaka majira ya saa 8:50 saa za Zambia na kumpokea mgeni wake Rais Samia Suluhu Hassan aliyewasili hapo saa 9:02.

ZAMBIA; Lusaka. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiweka shada la maua kwenye kaburi la Rais wa Kwanza wa Zambia Hayati Kenneth Kaunda (Presidential Burial site, Embassy Park) jijini Lusaka leo Oktoba 24, 2023. (Picha na Ikulu).

Shughuli hiyo iliambatana na sherehe za miaka 59 ya Uhuru Zambia yenye kauli mbiu Kuharakisha maendeleo ya Taifa kupitia rasilimali zilizopo.

Baada ya mapokezi, kabla ya kuweka mashada kulifanyika dua ya kuwaombea mashujaa wote waliojitolea kupigania nchi yao ya Zambia.

Baada ya dua hiyo alianza Rais Samia kuweka mashada katika mnara wa mashujaa na kufuatiwa na Rais wa Zambia.

Rais Samia aliambatana na mawaziri ambao ni Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba, Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Viwanda na Biasjara Dk Ashatu Kijaji na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga.

 

Habari Zifananazo

Back to top button