Rais Samia: Kila mtu atunze Demokrasia

‘ukija uwe msafi…ukipambana nitakubana’

RAIS Samia Suluhu amesema ni jukumu la kila mmoja kutunza utawala bora na kwamba hajaona taifa lolote ambalo linakiuka misingi ya utawala bora limefanikiwa.

Rais Samia ameyasema hayo leo Novemba 24, 2022 jijini Arusha akifungua mkutano wa 27 wa mwaka wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki (EALS).

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza katika mkutano wa 27 wa mwaka wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki (EALS)

Amesema mafanikio yoyote ya kiuchumi yanayokiuka misingi ya haki hayawezi kuwa endelevu kwa kuwa kwenye makaratasi uchumi utaonekana umekua lakini hautaakisi maisha ya wananchi wa kawaida.

“Hata kama taifa hilo lipo linaloendelea, DGP nzuri, kila kitu huku juu kizuri lakini watu wabovu nisingependa taifa hilo kuwa sehemu ya Afrika Mashariki, yabakie mbali huko yasiwe kwetu” amesema Rais Samia.

Amesema kila mtanzania na mwana jumuiya ya Afrika Mashariki anao wajibu wa kukuza utawala bora na kutetea haki za binadamu, na kwamba katika maisha yake hajawahi kuona Taifa lililofikia mageuzi ya kweli ya kiuchumi kwa kukiuka utawala wa kisheria.

Aidha, Rais Samia amesema  Tanzania inafuata misingi ya utawala bora na kwamba serikali yake itajitahidi kuijenga Tanzania yenye haki, demokrasia usawa na mafanikio.

“Na ndio maana kipindi hiki tumekuja na R nne, reconciliation, resilience, reform and rebuilding na tumeshaanza na reconciliation among ourselves ndio maana  mnasikia Tanzania imekaa vizuri.

“Wapi kuna ‘gap’ tukosoane, tukubali kukosoana twende pamoja ibara ya 8 (1)ya Katiba ya  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazingatia misingi ya kidemokrasia na haki ya kijamii.

Amesema pia masuala hayo yapo kwenye mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Ibara ya 6 Jumuiya ya Afrika Mashariki inaeleza utawala bora, utawala wa sheria, uwajibikaji na uwazi. Anayekwenda kinyume kwenye ‘Summit’ anakalishwa na kusemwa ili kurudi kwenye mstari.

Rais Samia amesema kuna umuhimu wa kufanya kazi pamoja na kuzitaka Jumuiya za  Wanasheria kuangalia sheria za nchi zao na namna ambavyo wataweza kupata fursa.

“Wakati mwingi serikali hatuwashiriki sana, ukiacha wale wale wanasheria wa  serikali, kila decision kuna rational, sasa kuna sababu zipi serikali iache kuhusisha jumuiya zao za ndani, kwa mfano miaka minne, mitano iliyopita, frankly speaking  TLS haikua chama cha wanasheria bali chama cha wanaharakati, na mapambano yao ilikuwa dhidi ya serikali.

“Sasa nikishakujua wewe ni dhidi angu nitakushirikishaje?  nikikuona una sura ya uadui nami sitakushirikisha,  mpaka nikuone unaonyesha am here to support you, am here to save the country, am here kuonyesha ujuzi wangu nikikuona unaonyesha hivyo nitakushirikisha.

“Utatumia sheria zote za kimataifa na mimi nitatumia zangu za ndani kukuvaa usishiriki kwangu….; ‘Kama unataka kuja kwangu kufanya kazi uje ukiwa msafi, usinitegeshee, mine clean, come clean let go together.’

Awali, akizungumza Rais wa EALS Bernard Haundo amesema chama hicho kinaamini mafanikio ya nchi za EAC yatatokana na watu wake kuungana wakiwemo wanasheria jambo ambalo pia lilikuwa ni ndoto ya waasisi wa jumuiya hiyo akiwemo baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button