Rais Samia kufanya ziara India

WAKATI Rais Samia Suluhu Hassan akitarajia kufanya ziara ya kitaifa ya siku nne nchini kiwango cha biashara kati ya Tanzania na India kimetajwa kuwa ni Dola bilioni 3.14 mwaka 2020 ikilinganishwa na Dola bilioni 2.14 mwaka 2017.

India inauza zaidi kwa Tanzania kwa tofauti ya Dola milioni 500.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba leo Oktoba 5, 2023 jijini Dar es Salaam. Makamba amesema ziara hiyo itaanza kuanzia Oktoba 8 hadi 11 mwaka huu.

Advertisement

Amesema, ziara hiyo inafanyika ikiwa imepita miaka minane tangu ziara ya mwisho ya kiongozi wa Tanzania kutembelea nchini India.

Amesema, madhumuni ya ziara hiyo ni kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliokuwepo wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili hususani kwenye sekta za kimkakati ikiwemo viwanda, afya, elimu, biashara, ulinzi na usalama, uchumi wa buluu, sekta ya maji na sekta ya kilimo.

Makamba amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kutafuta fursa za biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji kutoka India kuja kuwekeza nchini kwa kuwa India ni nchi kubwa na ina mtaji mkubwa, hivyo itasaidia kukuza biashara inayokua kwa kasi kati ya nchi hizo mbili.

Kwa mujibu wa Makamba, ziara hiyo ya Rais Samia inatarajiwa kuleta manufaa kadha wa kadha kwa Tanzania ikiwemo Watanzania kupata fursa za mafunzo katika nyanja mbalimbali nchini India na itazaa nafasi 1,000 za mafunzo katika sekta mbalimbali.

4 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *