Rais Samia kuhutubia taifa leo
RAIS Samia Suluhu Hassan leo anatarajiwa kulihutubia taifa wakati akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema mkutano huo ni moja ya hatua kubwa ambayo Rais Samia anaichukua kuhakikisha nchi inaendelea kurejea katika amani.
Chalamila aliwaeleza waandishi wa habari ofisini kwake mkutano huo unarejesha matumaini na kuendelea kuponya walipoumia Watanzania.
SOMA: Rais Samia aunda Tume Huru kuchunguza vurugu za uchaguzi
Alisema mkutano huo ni hatua ya kuhakikisha nchi inakuwa kitu kimoja, kujenga umoja na kusimamia taswira njema nje ya taifa na kuendelea kukuza na kuimarisha diplomasia yake na kuhakikisha nchi inaendelea kuwa kivutio cha uwekezaji kwa mataifa mengine.
Chalamila alisema mkoa huo una dhamana ya kuendelea kulinda amani kutokana na umuhimu wake hivyo ukiharibiwa utahatarisha si tu amani bali pia kusitisha huduma kwenda mikoa mingine au kutoka mikoa mingine kuingia Dar es Salaam.
“Sasa ni muda wa kujenga taifa letu pamoja, kulumbana kwa hoja na si kulumbana kwa kuharibu miundombinu au la kwa kufanya fujo zinazoweza kusababisha maumivu hata kukatisha uhai wa watu,” alisema.
Aliongeza: “Bado tunaendelea kuita Dar es Salaam kuwa ni kitovu cha amani, umoja, kiuchumi, kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa hivyo mtu yeyote anayodhamana pana ya kuhakikisha taswira zote zinalindwa kwa nguvu zote.”
Chalamila alisema mkoa huo unaendelea kurejea kwenye hali ya amani lakini pia maelekezo ya Rais Samia na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kupitia ziara zake yameendelea kutekelezwa.
Alitaja baadhi ya maelekezo hayo ni kuendelea kukarabati miundombinu ya barabara na kurejesha huduma mahali palipokuwa pamesimama.
Chalamila alisema ukarabati umeanza na muda si mrefu mabasi yote ya mwendokasi yatarejea barabarani kuendelea na utoaji wa huduma.
Alitoa mwito kwa wananchi watakapoona vyombo vya dola kwenye maeneo yao watoe ushirikiano na pale
wanapodhani kuna makundi ambayo hayaeleweki watoe taarifa serikali za mitaa.



