Rais Samia mgeni rasmi mkesha wa kuombea amani

Rais Samia mgeni rasmi mkesha wa kuombea amani

RAIS Dk Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkesha wa Mwaka Mpya kesho Desemba 31, 2022 wa kuiombea nchi iendelee kuwa na amani na utulivu.

Akizungumza leo Desemba 30, 2022 jijini Dar es Salaam,  Mwenyekiti wa Mkesha Mkubwa wa Kitaifa, Dua Maalum Dar es Salaam,  Mchungaji Derrick Luhende, amesema mkesha huo ni maalum kwa Taifa la Tanzania na  una malengo manne

Amesema lengo la kwanza ni kumuombea  Rais Samia jukumu la kuongoza Taifa  la Tanzania kwa hekima.

Advertisement

“Tunaiombea serikali na viongozi wote wa nchi yetu Mungu awape hekima na maarifa,” amesema.

Amesema viongozi wa kiroho wana wajibu wa kuileta nchi pamoja kwa kumuombea hekima Rais na watawala wote, ili Tanzania iendelee kuishi kwa amani na utulivu.

“Hakuna amani bila Mungu, yeye ndiye mtoa amani kwa watu wote wamchao kwa kusudi lake, Mungu analo kusudi na Taifa hili na ndio maana ametoa amani hii tulionayo leo, nyakati 2: 7-14,” amesema Luhende na kunukuu kifungu cha biblia

Amesema lengo la pili ni kuombea Taifa juu ya mmomonyoko wa maadili, kuombea familia, ndoa na watoto.

“Sasa hivi kumekua na mmomonyoko mkubwa wa maadili kwenye ndoa zinavunjika hovyo, vitendo vya ukatili kuuana kwa kisingizio cha wivu wa mapenzi hizi ni roho chafu inabidi tuziombee na kuzikemea.

“Tutaombea familia na watoto wetu, watoto wanabakwa, wanalawitiwa, watoto wanakuwa mashoga na wengine wasagaji hizi ni laana, tusipoomba tutakuwa taifa la ajabu, kizazi kisicho na maadili ni laana, tukeshe tuombeeni watoto wetu,” amesema.

Amesema lengo la tatu la mkesha huo ni kuombea umoja wa kitaifa, watu wasichanganye na siasa wala itikadi na lengo la nne ni  kumuomba Mungu aliepushe taifa la Tanzania na majanga ya ukame, magonjwa ya mlipuko, mafuriko ili uchumi wa Taifa ukue na uwe imara.

Mchungaji Luhende amesema kitaifa mkesha huo utafanyika kwenye viwanja vya Nyerere Square mjini Dodoma, ambapo Rais Samia atakuwa mgeni rasmi, wakati kwa Dar es Salaam utafanyika uwanja wa Uhuru na mgeni rasmi akiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu George Simbachawene.

Pia litafanyika Arusha uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Moshi Uwanja wa Majengo na Singida Uwanja wa Mtumbili.

Naye  Vicky Derrick akizungumzia mkesha huo amesema, amani ni  msingi wa maisha ya mwanadamu, bila amani maisha yanakuwa magumu, mtu hana usalama na mtu mwingine, kazi na shughuli za kila siku zinakwama, taifa lisilo na amani haliwezi kusonga mbele kimaendeleo hata lifikie malengo yake.

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *